WMA YASISITIZA MIZANI SAHIHJ KULINDA WAFANYABIASHARA NA MAPATO YA SERIKALI
Na Wellu Mtaki, Geita
Matumizi ya mizani sahihi na iliyohakikiwa yameendelea kusisitizwa kwa wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini, huku Wakala wa Vipimo (WMA) ukieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuzuia udanganyifu, kulinda maslahi ya wafanyabiashara na kuhakikisha Serikali inakusanya mapato yanayostahili kutokana na biashara ya madini.
Akizungumza katika Maonesho ya Sheria ya Madini yanayoendelea mkoani Mwanza, Meneja wa WMA Mkoa wa Mwanza, Karimu Zuberi, alisema Wakala huo umeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kuwaelimisha wadau wa madini kuhusu majukumu yake pamoja na umuhimu wa matumizi ya vipimo sahihi katika shughuli zao.
Alisema WMA ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara yenye jukumu kubwa la kumlinda mlaji, huku pia ikilinda watoa huduma na wafanyabiashara kwa kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika miamala ni sahihi.
“Tumekuja hapa kuwaelimisha wadau wetu hasa wa madini kuhusu majukumu yetu yanayohusu vipimo. Tunamlinda mlaji, lakini pia tunamlinda anayetoa huduma kwa kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara vina usahihi,” alisema Zuberi.
Alisema katika sekta ya madini kuna aina mbalimbali za vipimo vinavyotumika, ikiwemo mizani kwa ajili ya kupima madini, mita za maji, mita za umeme pamoja na mita za kupimia mafuta yanayotumika katika mitambo ya uchimbaji.
Kwa mujibu wa Zuberi, mita za maji na umeme zinazotumiwa na wachimbaji zinapaswa kuhakikiwa ili kuhakikisha matumizi yanayopimwa ni sahihi na kuepusha mtumiaji kulipa gharama zisizoendana na matumizi halisi.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kutumia mizani iliyohakikiwa na WMA kwa mujibu wa sheria, akisema mizani hiyo inapaswa kuhakikiwa angalau mara moja kwa mwaka.
Alisema matumizi ya mizani ambayo haijahakikiwa ni kinyume cha sheria na yanaweza kusababisha mhusika kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutozwa faini au adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria.
“Wote wanaotumia mizani katika biashara ya madini wanapaswa kuhakikisha mizani yao imehakikiwa na Wakala wa Vipimo. Mizani inapaswa kuhakikiwa angalau mara moja kwa mwaka,” alisema.
Zuberi alisema matumizi ya mizani sahihi yana umuhimu mkubwa katika kuzuia wizi na udanganyifu katika biashara ya madini, kwa kuwa tofauti ndogo katika uzito wa madini inaweza kusababisha hasara kubwa kwa muuzaji au mnunuzi.
Alisema kwa madini yanayouzwa kwa kuzingatia uzito, ikiwemo dhahabu na madini ya vito, usahihi wa mizani ni muhimu ili kuhakikisha kila upande anapata thamani inayolingana na kiasi halisi cha madini kilichopimwa.
Pia alisema vipimo sahihi vina mchango katika kulinda mapato ya Serikali, kwa kuwa madini yanapopimwa kwa usahihi, Serikali inaweza kupata mapato stahiki kupitia mrabaha, kodi na tozo nyingine zinazohusiana na biashara ya madini.
“Madini yanapaswa kupimwa kwa mzani ambao umehakikiwa na Wakala wa Vipimo ili kuhakikisha uzito unaotangazwa ni sahihi. Kama mzani si sahihi, Serikali inaweza kupoteza mapato yake na thamani ya madini pia inaweza kupotea bila kulipiwa kodi na mapato mengine,” alisema.
Aliongeza kuwa matumizi ya vipimo sahihi ni muhimu pia katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuaminika katika masoko ya madini, kwa kuwa biashara ya kimataifa inahitaji bidhaa kupimwa kwa viwango vinavyokubalika.
WMA imewataka wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta ya madini kuhakikisha vifaa vyao vya kupimia vinahakikiwa kwa wakati na kutumia vipimo vilivyothibitishwa kisheria ili kujenga mazingira ya biashara yenye uwazi, haki na kuaminiana.
