📍 GEITA | WAZIRI SANGU AIPONGEZA GGM KWA AJIRA HALALI ZA WAFANYAKAZI NA KUZINGATIA VIWANGO VYA KAZI
Na Wellu Mtaki, Geita
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGM) kwa kuendelea kutoa ajira kwa Watanzania, huku ikizingatia viwango vya kazi, usalama na afya mahali pa kazi pamoja na kuhakikisha michango ya wafanyakazi inawasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Sangu ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea banda la GGM katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, akisema alichokiona katika banda hilo kinaonesha namna kampuni hiyo inavyotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na haki za wafanyakazi.
Amesema GGM haijaangalia suala la ajira pekee, bali pia imekuwa ikihakikisha haki na ustawi wa wafanyakazi wake vinazingatiwa. Miongoni mwa hatua hizo ni ufadhili wa ujenzi wa Ofisi ya Tume ya Usuluhishi na Upatanishi (CMA), ambayo kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za kukamilika.
