Breaking News

COPRA YAWAFIKIA WAKULIMA, WAFANYABIASHARA ELIMU YA BIASHARA YA MAZAO

Na, Wellu Mtaki, Manyara

Wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya nafaka mkoani Manyara wametakiwa kuzingatia taratibu za usajili, upatikanaji wa vibali na kanuni za biashara ya mazao ili kuongeza tija katika shughuli zao na kunufaika zaidi na masoko.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) Kanda ya kati Andrew Mgaya  kupitia ushiriki wake katika maonyesho ya kilimo na biashara, yanayolenga kuwafikia wadau wa sekta hiyo na kuwapa elimu kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo pamoja na taratibu zinazopaswa kufuatwa katika biashara ya mazao.

 kupitia banda la COPRA Mgaya  ametoa elimu kwa wakulima na wafanyabiashara kuhusu namna ya kusajili shughuli zao, kupata vibali vya kununua na kuuza mazao, pamoja na kufahamu taratibu mbalimbali zinazohusiana na biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko.

Mgaya amesema mamlaka hiyo imeona umuhimu wa kushiriki ili kuwapa wadau fursa ya kupata maelezo ya moja kwa moja kuhusu huduma zinazotolewa, hatua zinazopaswa kufuatwa na namna ya kutatua changamoto zinazowakabili katika shughuli zao.

Amesema ushiriki huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya COPRA na taasisi nyingine pamoja na wadau wa sekta ya kilimo na biashara, ili kuboresha mazingira ya uzalishaji na biashara ya mazao nchini.

Aidha, katika banda hilo kunaoneshwa sampuli za mazao yanayolimwa katika maeneo mbalimbali, yakiwemo mbaazi, dengu na mazao mengine yanayolimwa mkoani Manyara na maeneo jirani.

Amesema mazao hayo yana nafasi muhimu katika kuongeza kipato cha wakulima na kuchochea shughuli za kiuchumi, hivyo ni muhimu kwa wakulima kupewa elimu kuhusu mbinu bora za uzalishaji, utunzaji wa mazao baada ya kuvuna na namna ya kuyafikisha sokoni yakiwa katika hali inayokidhi mahitaji ya wanunuzi.

Ameongeza kuwa wakulima na wafanyabiashara wanaohitaji maelezo kuhusu usajili, vibali na taratibu za biashara ya mazao wanakaribishwa kutembelea banda la COPRA ili kupata ufafanuzi na mwongozo unaohitajika.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, elimu inayotolewa inalenga kuwasaidia wadau kufahamu wajibu wao na kufanya biashara kwa kufuata taratibu zilizowekwa, hatua inayoweza kuchangia kuimarika kwa biashara ya mazao na kuongeza manufaa kwa wananchi wanaojihusisha na kilimo.