Breaking News

SERIKALI YATAKA MAZINGIRA BORA YA KUKUZA STARTUPS

 


Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Serikali imesisitiza umuhimu wa kuboresha sera na mazingira ya biashara kwa kampuni changa za ubunifu (startups) ili ziweze kukua, kuzalisha ajira na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Hayo yameelezwa katika Tanzania Startup Week 2026 inayofanyika Dar es Salaam, ambapo viongozi wa Serikali na wadau wa sekta ya ubunifu wamejadili namna ya kuwezesha mawazo ya vijana kubadilika kuwa biashara endelevu zenye uwezo wa kukua.

Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesisitiza umuhimu wa kuwa na sera zinazolenga kuimarisha mfumo wa kampuni changa na kuweka mazingira yatakayowezesha sekta hiyo kuchangia maendeleo ya uchumi.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kurahisisha mifumo ya kiutendaji na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi.

 Amesema taasisi na wizara zinapaswa kupitia sheria, taratibu na mifumo yao ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuwawezesha wafanyabiashara kupata huduma kwa urahisi.

Naye Mtendaji Mkuu wa Tanzania Startup Association, Zahoro Muhaji, amesema kampuni changa bado zinakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mitaji, masoko na kanuni za biashara, huku Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Paul Makanza, akisisitiza umuhimu wa kuwaunganisha wajasiriamali na wawekezaji pamoja na kuanzisha maeneo maalumu ya ubunifu yatakayosaidia mawazo ya vijana kupata mitaji na fursa za kukua.