Breaking News

TAHILISO YATAKA VYAMA VYA SIASA KUTANGULIZA MASLAHI YA TAIFA

 


Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHILISO), Geoffrey Kiliba, ametoa wito kwa vyama vya siasa nchini kuimarisha mijadala yenye hoja na kuhakikisha maslahi ya taifa yanakuwa msingi wa shughuli zao za kisiasa.

Akizungumza leo Oktoba 20, 2026 jijini Dar es Salaam, Kiliba amesema mfumo wa vyama vingi ulioanzishwa mwaka 1992 ulilenga kujenga ushindani wa mawazo na kuimarisha demokrasia, hivyo viongozi wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa kuzingatia maendeleo na umoja wa wananchi.

Amesema baada ya zaidi ya miongo mitatu ya mfumo wa vyama vingi, kuna umuhimu wa wanasiasa kuheshimu maoni yanayotofautiana, kutumia lugha za staha na kuepuka kauli zinazoweza kuongeza migawanyiko miongoni mwa wananchi.

Kiliba pia amesisitiza umuhimu wa vyama vya siasa kushiriki katika mchakato wa Katiba mpya pamoja na kutoa mapendekezo yanayolenga kutatua changamoto za wananchi katika sekta za elimu, afya, nishati na usafiri. Amesema tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa kikwazo cha viongozi kuonyesha utu wakati wa misiba na majanga.

Akizungumzia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kiliba amehoji hatua zilizochukuliwa na chama hicho katika kukabiliana na changamoto ambacho kimekuwa kikizizungumzia, akisisitiza kuwa demokrasia imara inahitaji ukweli, uwajibikaji, kuheshimu mitazamo tofauti na kulinda umoja wa taifa.