Breaking News

MBOLEA YA MIAMBA YALENGA KUREJESHA RUTUBA YA UDONGO, KUONGEZA MAVUNO


Wakulima wametakiwa kuzingatia matumizi ya mbolea zinazolenga kurejesha rutuba ya udongo na kuimarisha uzalishaji wa mazao, ili kukabiliana na changamoto ya kupungua kwa rutuba ya ardhi na kuongeza upatikanaji wa chakula bora nchini.

Wito huo umetolewa na Donald George Mwakamele, mtaalamu wa utengenezaji wa mbolea zinazotokana na miamba, anayefanya shughuli zake mkoani Songwe, akieleza kuwa mbolea hiyo imetengenezwa kwa kutumia miamba yenye madini mbalimbali yanayoweza kusaidia kuboresha hali ya udongo na ukuaji wa mimea.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani, yaliyobeba kaulimbiu inayohimiza ubunifu wa leo kwa lishe bora ya kesho, Mwakamele alisema matumizi ya mbolea hiyo yanalenga kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji huku wakizingatia afya ya udongo kwa muda mrefu.

Alisema udongo unapokuwa na upungufu wa virutubisho, uwezo wake wa kuzalisha mazao hupungua, hivyo ni muhimu kwa wakulima kutafuta njia zinazoweza kurejesha madini na kuboresha rutuba ya ardhi wanayotumia kwa kilimo.

“Mbolea hii inatengenezwa kutokana na miamba yenye madini ya aina mbalimbali. Lengo ni kusaidia kurejesha virutubisho katika udongo na kuuwezesha kuwa na uwezo mzuri wa kustawisha mimea,” alisema Mwakamele.

Aliongeza kuwa matumizi ya mbolea hiyo yamefanyiwa majaribio katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Moshi, Njombe, Songwe na Songea, akieleza kuwa imeonyesha matokeo mazuri katika baadhi ya mazao, yakiwemo mazao ya kimkakati.

Kwa mujibu wa Mwakamele, ubunifu huo unaweza kuwa sehemu ya jitihada za kuongeza tija katika kilimo na kuwasaidia wakulima kupata mazao yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.

Alisema kurejesha rutuba ya udongo ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa ardhi inaendelea kuwa na uwezo wa kuzalisha chakula kwa vizazi vya sasa na vijavyo, huku akiwahimiza wakulima kuzingatia aina ya mbolea wanazotumia na mahitaji halisi ya udongo wao.

Mwakamele alisisitiza kuwa maendeleo ya kilimo yanahitaji ubunifu unaozingatia uhifadhi wa rasilimali za asili, akieleza kuwa udongo wenye rutuba ni msingi wa uzalishaji wa mazao na upatikanaji wa lishe bora kwa jamii.

Hata hivyo, alibainisha kuwa matumizi ya mbolea yanapaswa kuzingatia mahitaji ya udongo na zao husika, akiwahimiza wakulima kutafuta ushauri wa kitaalamu ili kuhakikisha wanatumia virutubisho vinavyofaa kwa mashamba yao.