Breaking News

UPUNGUFU WA MAZIWA WATIKISA SOKO, WAFUGAJI WATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI

 


Na. Wellu Mtaki,Tanga

Tanzania inazalisha wastani wa lita bilioni 4.2 za maziwa kwa mwaka, kiwango ambacho bado kiko chini ya mahitaji yanayokadiriwa kufikia lita bilioni 13, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuimarisha upatikanaji wa maziwa kwa ajili ya lishe bora.

Kutokana na hali hiyo, Bodi ya Maziwa Tanzania imewataka wafugaji, wawekezaji na wadau wa sekta binafsi kuongeza uzalishaji na uwekezaji katika tasnia ya maziwa ili kupunguza pengo hilo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, Meneja Masoko wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Joseph Semu, amesema maziwa yana virutubishi muhimu, ikiwemo protini na madini, vinavyosaidia ukuaji na kuimarisha mwili.

Amesema ni muhimu familia kuzingatia lishe bora kwa kuwajumuishia watoto maziwa katika mlo wao, kulingana na mahitaji yao ya lishe, ili kuwasaidia kupata virutubishi vinavyohitajika kwa ukuaji na maendeleo yao.

Semu ameeleza kuwa elimu kwa wananchi kuhusu faida za maziwa inapaswa kuendelea kutolewa ili kujenga utamaduni wa kuyatumia kama sehemu ya mlo wa kila siku, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora na usalama wa maziwa yanayotumiwa.

Amesema tofauti kati ya uzalishaji wa sasa na mahitaji ya maziwa nchini inaonesha kuwa bado kuna fursa kubwa ya uwekezaji katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ukusanyaji na uchakataji wa maziwa pamoja na shughuli nyingine zinazohusiana na tasnia hiyo.

Kwa mujibu wa Semu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanzisha mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa unaolenga kuongeza uzalishaji na kuboresha mifumo ya ukusanyaji na uchakataji wa maziwa.

Amesema juhudi hizo pia zinahusisha kuboresha mifumo ya uzalishaji wa mifugo ili wafugaji wapate ng’ombe wenye uwezo mkubwa wa kutoa maziwa, hatua inayotarajiwa kuongeza tija na kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa kila lita.

Aidha, amewahimiza wawekezaji kuwekeza katika ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa, viwanda vya kuchakata maziwa na uzalishaji wa vifungashio pamoja na vifaa vya viwandani vinavyohitajika katika tasnia hiyo.

Amesema uwekezaji katika maeneo hayo unaweza kuongeza upatikanaji wa maziwa, kuboresha ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kufungua fursa za ajira na biashara kwa wananchi.

Hatua ya kuongeza uzalishaji na matumizi ya maziwa inatajwa kuwa muhimu katika kuimarisha lishe ya familia na kukuza uchumi, hususan kwa wafugaji na wajasiriamali wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa maziwa nchini.