Breaking News

Waziri Mbarawa: Usafiri ni kichocheo cha biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi

 


Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam 

WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema usafiri si suala la kusafirisha watu na mizigo pekee, bali ni kichocheo muhimu cha biashara, uwekezaji, uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa taifa.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Usafiri, Usafirishaji na Menejimenti, ambapo amesema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya usafiri, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, uboreshaji wa bandari, kuimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), upanuzi wa mfumo wa mabasi yaendayo kwa kasi, uboreshaji wa barabara pamoja na kuendeleza usafiri wa majini na uchumi wa buluu.

“Lengo letu si kujenga miundombinu pekee, bali tunataka kujenga mfumo mmoja wa usafiri uliounganishwa, ambapo reli, barabara, viwanja vya ndege na usafiri wa majini vinafanya kazi kwa ufanisi,” amesema Prof. Mbarawa.

Amesema Tanzania inaendelea kujenga nafasi yake kama kitovu muhimu cha usafiri na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kusini, kupitia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu inayolenga kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za usafirishaji na muda wa mizigo kufika sokoni, pamoja na kuimarisha usalama na ubora wa huduma kwa wananchi.

Prof. Mbarawa amesema Serikali inalenga kutumia miundombinu ya usafiri kama kichocheo cha fursa zaidi za kiuchumi, hususan wakati Tanzania ikielekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Tunapoelekea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, tunahitaji mfumo wa usafiri unaosaidia Tanzania kuwa na uchumi shindani, kukuza viwanda na biashara, pamoja na kuimarisha uhusiano na masoko ya ndani na ya kimataifa,” amesema.

Aidha, Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa utafiti katika sekta ya usafiri na usafirishaji, akiwataka watafiti kuhakikisha tafiti zao hazibaki kwenye makaratasi, bali zinatumika kutatua changamoto halisi zinazokabili sekta hiyo.

Amesema utafiti unapaswa kusaidia kuboresha ufanisi wa bandari na reli, kuimarisha usalama wa usafiri, kuwezesha matumizi ya teknolojia mpya na kusaidia kujenga miundombinu inayoweza kuhimili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, ili kutoa matokeo yanayoonekana na yanayoaminika.

Kwa upande wake, Mhandisi Dkt. Prosper Mgaya amesema Mkutano huo umefikia hatua ya nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, ambapo mkutano wa kwanza ulikuwa na wawasilishaji wawili wa kimataifa, huku mwaka huu ukiwa na wawasilishaji 16 kutoka nje ya nchi.

Amesema mkutano wa mwaka huu umejikita zaidi katika kujadili usafiri janja, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika sekta ya reli, huku ukiwa na mada ndogo tano zinazolenga kujadili changamoto na fursa mbalimbali katika sekta ya usafiri na usafirishaji.

“Tunatambua Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya usafirishaji. Kupitia kongamano hili tunalenga kujadili na kutoa majibu ya changamoto zilizopo katika usafirishaji. Tunaiishukuru Wizara ya Uchukuzi kwa kuhakikisha kongamano hili linafanikiwa,” amesema Dkt. Mgaya.