WATANZANIA TUTANGAZE AMANI TULIYONAYO, SI KUIZUNGUMZIA KAMA HAIPO
Prof. Emmanuel Shija, Mkurugenzi Mkuu na Katibu wa Kamati ya Maadili ya Jumuiya ya Maridhiano Tanzania
Na Wellu Mtaki, Dodoma
Watanzania hawapaswi kuwa mstari wa mbele kuzungumzia kwamba nchi haina amani, bali wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutambua, kuthamini na kuitangaza amani iliyopo nchini, kwa kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo na ustawi wa taifa.
Hayo yamesemwa na Prof. Emmanuel Shija, Mkurugenzi Mkuu na Katibu wa Kamati ya Maadili ya Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, wakati wa hafla ya kumpongeza baada ya kutunukiwa Tuzo ya Amani Duniani.
Prof. Shija amesema Watanzania wanaposema kwa kujiamini kuwa Tanzania ni nchi yenye amani, wanajenga matumaini, mshikamano na kujiamini miongoni mwa wananchi, jambo ambalo ni muhimu katika kujenga taifa lenye nguvu na maendeleo endelevu.
Amewataka wananchi wote kuendelea kulinda, kutunza na kudumisha amani ya nchi, huku wakiepuka vitendo na kauli zinazoweza kuvuruga utulivu, mshikamano na umoja wa Watanzania.
Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na amani, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha tunu hiyo inalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
“Amani si jambo la kuchukulia kawaida; ni hazina, ni tunu na ni silaha yetu ya kujenga taifa. Bila amani, maendeleo hayawezi kuwa na msingi imara.”
Prof. Shija amesisitiza kuwa kila Mtanzania anapaswa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuhimiza umoja, kuheshimiana, kuvumiliana na kuishi kwa upendo na mshikamano.
Prof. Shija ashukuru kutunukiwa Tuzo ya Amani
Sambamba na hilo, Prof. Shija ametoa shukrani zake kwa kutunukiwa tuzo hiyo, akieleza kuwa kutambuliwa kwake ni jambo kubwa linaloacha historia nzuri katika jamii na kuongeza chachu ya kuendelea kuamini kwamba amani ndiyo msingi wa kila mafanikio ya taifa.
Amesema tuzo hiyo si heshima kwake binafsi pekee, bali pia ni ishara ya kuthamini juhudi zinazofanyika katika kuhamasisha amani, mshikamano na umoja katika jamii.
Kwa msingi huo, amewataka Watanzania wote kuchukua nafasi yao katika kuhakikisha amani inalindwa na kutunzwa.
“Amani ni yetu sote. Tuilinde, tuitunze na tuiache ikiwa imara kwa ajili ya watoto wetu na vizazi vijavyo.”
Amesema Tanzania ikiwa na amani, mshikamano na umoja, itaendelea kuwa na uwezo mkubwa wa kujenga taifa lenye matumaini, fursa na maendeleo kwa wote.
Kwa upande wake, Makamu Askofu wa Mkoa wa Dodoma, Mchungaji Daudi, amesema siku hiyo ilikuwa ya furaha na heshima kwa kuwa walipata fursa ya kumpongeza Prof. Shija kwa kutunukiwa Tuzo ya Amani Duniani.
Amesema viongozi na watumishi wa Mungu wamefurahishwa na kutambuliwa kwa Mtumishi mwenzao katika juhudi za kuhamasisha amani duniani.
“Leo ni siku ya kumpongeza Dkt. Shija kwa kutunukiwa Tuzo ya Amani. Tumefurahi kuona Mtumishi mwenzetu ametunukiwa tuzo ya amani inayotambulika duniani,” amesema.
Mchungaji Daudi amesema amani ni mafanikio na baraka katika maisha ya mwanadamu, akisisitiza kuwa bila amani hakuna maelewano wala mazingira mazuri ya kufanikisha maendeleo.
Amesema jukumu kubwa la viongozi wa dini na wachungaji ni kuendelea kuwafundisha waumini na jamii kwa ujumla umuhimu wa amani, pamoja na kuhimiza wananchi kuilinda kwa gharama yoyote.
“Usipokuwa na amani, hakuna maelewano na maendeleo hayawezi kuwepo. Jukumu kubwa sisi kama wachungaji ni kuwafundisha watu amani na kuilinda kwa gharama yoyote, kwa sababu amani ikivunjika, kuirejesha ni gharama,” amesema.
Amesisitiza kuwa juhudi za kulinda amani zinapaswa kuwa jukumu la kila mwananchi, kwa kuwa amani inapolindwa huweka mazingira bora ya umoja, mshikamano na maendeleo ya taifa.
