SUZA Yaja na Teknolojia Kuwasaidia Wavuvi na Wachimbaji Madini
Na Mwandishi wetu Tanga
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimekuja na teknolojia na tafiti mbalimbali zinazolenga kuwasaidia wavuvi na wachimbaji wadogo wa madini, ili kuweza kupata tija pamoja na kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za uzalishaji.
Akizungumza katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea Jijini Tanga, Makamu Mkuu wa Chuo hicho , Prof. Said Ali Hamad Vuai, amesema chuo hicho kinafanya utafiti wa soko la kimtandao kwa mazao ya uvuvi, unaolenga kuwaunganisha wavuvi na wanunuzi ndani na nje ya Tanzania.
Amesema teknolojia hiyo inalenga kuwawezesha wavuvi kupata masoko yenye tija kwa mazao yao, kuongeza kipato na kutumia fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Prof. Vuai amesema SUZA pia imefanya utafiti unaolenga kuboresha usalama wa wachimbaji wadogo wa madini, kwa kuwawezesha kupata msaada kwa wakati wanapokabiliwa na changamoto wakati wa shughuli za uchimbaji.
Amesema tafiti hizo ni sehemu ya juhudi za SUZA kutumia elimu, teknolojia na ubunifu kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi na kuchochea maendeleo ya Taifa.
“Tunataka elimu na tafiti tunazofanya ziwe na manufaa kwa jamii, zisaidie kutatua changamoto na kuongeza thamani katika shughuli za uzalishaji”.
Ameeleza kuwa mbali na tafiti na ubunifu, SUZA inatoa programu mbalimbali za elimu kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada na viwango vya juu vya kitaaluma katika maeneo ya teknolojia, afya, famasia, sayansi, kilimo, ufugaji, biashara, ujasiriamali, masoko, ununuzi na ugavi, elimu pamoja na uandishi wa habari.
Prof. Vuai amewataka wananchi wanaoshiriki Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kutembelea banda la SUZA ili kufahamu zaidi kuhusu teknolojia, tafiti na programu za elimu zinazotolewa na chuo hicho.
Amesema SUZA inaendelea kutoa fursa kwa vijana kutoka Tanzania na nje ya nchi kutumia elimu na ubunifu kama nyenzo ya kutatua changamoto za jamii na kujenga fursa za kiuchumi.
Mudrick Mohamed Iddi kutoka SUZA, amebuni teknolojia ya kuwasaidia wachimbaji madini kupeleka taarifa juu yeye awepo chini ya ardhi endapo atakumbwa na changamoto yoyote bila kutumia simu hivyo kutumia Mesh Network.

