Breaking News

RAIS SAMIA KUZINDUA RASMI JNHPP AGOSTI 22, 2026

Na Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM: 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) tarehe 22 Agosti 2026 katika eneo la mradi Rufiji, mkoani Pwani.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema uzinduzi huo utahudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania, wananchi pamoja na wadau wa maendeleo.

Amesema uzinduzi huo ni tukio muhimu katika historia ya Tanzania kutokana na mchango wa mradi huo katika kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa shughuli za uzalishaji, uwekezaji na ukuaji wa uchumi.

Mradi huo umegharimu takribani Shilingi trilioni 7.452 na umetekelezwa kwa fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Ndejembi amesema wakati wa ujenzi wake, mradi huo ulitoa ajira kwa takribani wafanyakazi 12,000, ambapo asilimia 99 walikuwa Watanzania.

Kwa sasa, uwezo wa mitambo yote ya kuzalisha umeme nchini umefikia takribani megawati 4,648, huku JNHPP ikiwa na mchango mkubwa katika kuongeza umeme unaoingia kwenye gridi ya Taifa.

Amesema hadi kufikia Mei 31, 2026, kituo hicho kilikuwa kimechangia takribani asilimia 44.9 ya umeme wote uliozalishwa na kuingia kwenye gridi ya Taifa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Aidha, amesema tangu kuanza kuzalisha umeme, JNHPP imeendelea kuongeza kiwango cha umeme kwenye gridi ya Taifa na kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa uzalishaji uliokuwa ukichangia mgao wa umeme.

Bwawa hilo lina uwezo wa kuhifadhi takribani mita za ujazo bilioni 33 za maji, ambayo ni rasilimali muhimu kwa shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo kilimo cha umwagiliaji, utalii na matumizi ya binadamu.

Waziri amesema uwekezaji huo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, pamoja na juhudi za Serikali kuongeza uzalishaji wa umeme, kuimarisha gridi ya Taifa na kuweka mazingira bora kwa shughuli za kiuchumi na uwekezaji.

Uzinduzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 22, 2026, unatajwa kuwa hatua muhimu katika historia ya sekta ya nishati nchini Tanzania.