SERIKALI YAWATAKA MAAFISA KAZI KUIMARISHA USIMAMIZI WA SHERIA ZA KAZI
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
Serikali imewataka Maafisa Kazi nchini kuimarisha usimamizi wa sheria za kazi, kufanya kaguzi zenye tija na kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi, hatua inayolenga kujenga mahusiano bora na kuongeza ufanisi katika maeneo ya kazi.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 4, 2026, jijini Dodoma na Kamishna wa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Susan Mkangwa, wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Kazi kwa mwaka wa fedha 2025/26, kilichowakutanisha Maafisa Kazi Wafawidhi wa Ofisi hiyo.
Mkangwa amesema kikao hicho kina lengo la kutathmini utekelezaji wa majukumu yaliyofanyika katika mwaka wa fedha uliopita, kupitia mpango kazi wa mwaka 2026/27, pamoja na kujengeana uwezo katika masuala ya utekelezaji wa sheria za kazi, utawala, taarifa za soko la ajira na masuala ya fidia kwa wafanyakazi.
Amesema kikao hicho pia kinatoa fursa kwa watumishi kutafakari mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Kazi katika mwaka mpya wa fedha.
Aidha, amewapongeza Maafisa Kazi hao kwa mafanikio waliyoyapata katika mwaka wa fedha uliopita, ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa amri ya kima cha chini cha mshahara, kuimarisha ushirikishwaji wa wafanyakazi kupitia mabaraza ya wafanyakazi, kuratibu mashauriano kati ya Serikali, waajiri na vyama vya wafanyakazi, pamoja na kusimamia na kuratibu ajira za wageni.
Hata hivyo, Mkangwa amewahasa Maafisa Kazi hao kuendelea kuimarisha usimamizi wa sheria katika maeneo ya kazi, huku akiwataka kufanya kaguzi zinazolenga kuleta matokeo chanya na kuboresha mazingira ya kazi.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia yanapaswa kupewa kipaumbele, akiwataka watumishi kutumia kikamilifu Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Soko la Ajira, ambao utasaidia kuboresha upatikanaji na usimamizi wa taarifa za soko la ajira nchini.
Akizungumza awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, amesema WCF inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano kupitia Idara ya Kazi, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu haki, wajibu na taratibu za kupata fidia pindi wanapopata ajali, kuugua au kufariki kutokana na kazi
Amesema ushirikiano huo unalenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu na uelewa kuhusu mfumo wa fidia, pamoja na kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wadau wa soko la ajira katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mikoa na wilaya ambazo WCF haina ofisi za moja kwa moja.



