TALGWU: HATUNA UGOMVI NA SERIKALI, TUNASHIRIKIANA KUTETEA HAKI ZA WAFANYAKAZI
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimesema hakina mgogoro wala ugomvi na Serikali, bali kinaendelea kushirikiana nayo kwa karibu katika kuhakikisha haki na maslahi ya wafanyakazi yanapatikana kwa wakati na kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizopo nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa TALGWU, Festo Mbakilwa, wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wafanyakazi wa chama hicho uliofanyika mkoani Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulikuwa na agenda ya kuwachagua viongozi wapya wa chama.
Mbakilwa amesema ushirikiano mzuri kati ya Serikali na chama hicho ni muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi, akieleza kuwa njia bora ya kusimamia haki za mfanyakazi ni kwa pande husika kukaa pamoja na kujadiliana kwa lengo la kupata suluhisho lenye tija.
“Sisi hatuna ugomvi na Serikali, tunashirikiana na Serikali. Hakuna kitu kizuri kama kusimamia haki ya mfanyakazi kwa kukaa mezani na kujadiliana,” amesema Mbakilwa.
Amesema Serikali imekuwa ikishirikiana vyema na TALGWU katika kuhakikisha changamoto na masuala yanayohusu haki za wafanyakazi yanapatiwa ufumbuzi kwa haraka na kwa wepesi.
Katika hatua nyingine, Mbakilwa amewataka wanachama wa TALGWU kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa kuchagua viongozi bora, waadilifu na wenye uwezo wa kuiongoza chama kwa manufaa ya wanachama, Serikali na chama kwa ujumla.
Amesema uchaguzi unapaswa kufanyika kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na taratibu zilizowekwa katika katiba ya chama, akisisitiza kuwa matumizi ya njia zisizo sahihi yanaweza kusababisha migogoro na changamoto ndani ya chama.
“Mnapokwenda kuchaguana, mchague kwa njia nzuri na si kwa njia mbaya. Njia nzuri itawaletea kiongozi bora ambaye atakwenda kukisaidia chama na Serikali,” amesema.
Ameongeza kuwa uchaguzi unaozingatia haki, usawa na demokrasia ndio msingi wa kupata viongozi wanaoweza kusimamia ipasavyo maslahi ya wafanyakazi.
“Ukitumia njia mbaya italeta changamoto ambazo zinaweza kuleta madhara ndani ya chama na Serikali kwa ujumla,” amesema.
Mbakilwa pia amesisitiza umuhimu wa kutatua migogoro na changamoto za wafanyakazi kupitia mazungumzo na majadiliano badala ya kukimbilia kutumia sheria katika kila jambo.
Amesema kukaa pamoja mezani na kujadiliana kunaweza kusaidia kupata suluhisho la haki na lenye tija kwa pande zote, huku akionya kuwa matumizi yasiyo sahihi ya sheria yanaweza kuongeza changamoto badala ya kuzitatua.
“Hakuna kitu kizuri kama kusimamia haki ya mfanyakazi kwa kukaa mezani. Ukitaka kusimamia sheria kila wakati, ipo siku sheria inaweza kukutia aibu, kwa sababu siku utakutana na sheria yenye makali,” amesema.
Aidha, amewataka wanachama kuendelea kujenga utamaduni wa kushirikiana na kukiweka chama katika mazingira yatakayomfanya kila mwanachama ajisikie kuwa sehemu muhimu ya chama hicho.
Kwa upande wake, Katibu wa TALGWU, Audax Stephano, amesema chama hicho kina utaratibu wa kufanya uchaguzi wa viongozi kila baada ya miaka mitano, huku Mkutano Mkuu ukifanyika kila mwaka kwa mujibu wa katiba ya chama.
Amesema mkutano huo pia unatoa fursa kwa chama kuwasilisha taarifa mbalimbali, ikiwemo taarifa za mapato na matumizi pamoja na mambo mengine yanayohusu maendeleo na uendeshaji wa chama.
“Kama katiba yetu inavyotutaka, tunakutana kila mwaka na kufanya Mkutano Mkuu wa mwaka. Kwa ajili ya uchaguzi, pamoja na kutoa taarifa ya mapato na matumizi ,” amesema
Stephano ameipongeza Serikali kwa juhudi inazofanya katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao na mazingira bora ya kutekeleza majukumu yao.
Amesema zoezi la uchaguzi linaendelea vizuri na ameeleza matumaini yake kuwa mchakato huo utaendelea kuzingatia haki, usawa na misingi ya demokrasia.
“Tunaipongeza Serikali kwa kusaidia wafanyakazi. Wamekuwa wakifanya kazi kwa uhuru na kwa kuzingatia taratibu zilizopo nchini. Zoezi linaendelea vizuri na ninaamini haki na demokrasia zitatumika,” amesema Stephano

