EWURA YAWAHIMIZA WAWEKEZAJI KUJENGA VITUO VYA MAFUTA VIJIJINI
📍 GEITA
Na Wellu Mtaki, Geita
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewahimiza wawekezaji kutumia fursa ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini, ambapo masharti na gharama za leseni zimepunguzwa ili kuongeza upatikanaji wa huduma za mafuta na kudhibiti uuzaji holela wa bidhaa za petroli. Akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Nyirabu Musira, amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha uwekezaji katika maeneo ya vijijini.
Amesema gharama ya kuomba leseni ya kituo cha mafuta ni Sh50,000 kwa maeneo ya mjini na vijijini, huku leseni ya miaka mitano kwa kituo cha mjini ikiwa Sh1 milioni, wakati kwa kituo cha vijijini ni Sh100,000. Aidha, amesema EWURA imepunguza masharti ya ujenzi wa vituo vya vijijini kwa kutolazimisha viwe na muonekano na miundombinu inayofanana na vituo vikubwa vya mijini, hatua inayosaidia kupunguza gharama za uwekezaji.
Musira amesema EWURA pia imetumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na uvunaji wa maji ya mvua. Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa EWURA, Tobietha Makafu, amewataka mafundi umeme wasio na leseni kufika katika banda la mamlaka hiyo kupata elimu kuhusu taratibu za kupata leseni. Aidha, amesema EWURA inapokea malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za nishati na maji, ikiwemo huduma za TANESCO na mamlaka za maji.
EWURA imewahimiza wananchi wa Geita na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa kutembelea banda lake katika maonesho hayo ili kupata elimu kuhusu huduma za nishati na maji, fursa za uwekezaji, taratibu za kupata leseni pamoja na namna ya kuwasilisha malalamiko na kupata ufumbuzi.
