Breaking News

VETA GEITA YAJA NA VIATU MAALUM VYA KUWALINDA WACHIMBAJI DHIDI YA MAJANGA MIGODINI.

 


📍 GEITA

Na Wellu Mtaki, Geita

Katika Maonesho ya Tisa ya Madini yanayofanyika mkoani Geita, Chuo cha Ufundi Stadi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kimekuja na bidhaa mbalimbali za ngozi, ikiwemo viatu maalum vilivyotengenezwa kwa ubora na uimara kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji kujikinga dhidi ya majanga wanapokuwa katika shughuli za uchimbaji madini.

Akizungumza na Nico Media katika maonesho hayo, Mwalimu wa Bidhaa za Ngozi kutoka VETA, Hamidu Shabani, amesema chuo hicho kinaendelea kutoa mafunzo ya vitendo kwa wananchi katika fani mbalimbali, ikiwemo utengenezaji wa viatu vya usalama vinavyoweza kutumika katika maeneo ya kazi kama migodini.

Amesema viatu hivyo vimetengenezwa kwa kuzingatia mahitaji ya usalama kazini, ambapo vina chuma sehemu ya mbele ya vidole pamoja na bati maalum ndani ya unyayo, hatua inayolenga kumlinda mchimbaji dhidi ya majeraha yanayoweza kusababishwa na vitu vyenye ncha kali au kugongwa na vitu vizito.

“Katika sekta ya madini, suala la usalama mahali pa kazi ni muhimu. Wafanyakazi wanapaswa kutumia vifaa vya kujikinga wanapokuwa kazini. Viatu hivi vina chuma mbele ya vidole na bati ndani ya unyayo, hivyo vinasaidia kumlinda mchimbaji iwapo atakanyaga kitu chenye ncha kali au kugongwa na kitu kizito,” amesema Shabani.

Aidha, Shabani amesema VETA inaendelea na udahili wa wanafunzi kwa ajili ya mafunzo mbalimbali ya muda mrefu na Mfupi huku akiwataka wananchi kutumia fursa zinazotolewa na chuo hicho ili kujifunza ujuzi unaoweza kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Amesema udahili wa baadhi ya kozi ulianza mwezi Agosti mwaka huu, huku mafunzo ya muda mrefu yakitarajiwa kuanza mwakani.

VETA imeendelea kutoa wito kwa wananchi kutambua kuwa elimu ya ufundi stadi ni fursa kwa wote, bila kujali eneo au hali ya mtu, kwani ujuzi huo unaweza kuwa msingi wa kujiajiri na kujenga maisha.