SERIKALI YAPONGEZA TBA KWA KUPUNGUZA GHARAMA ZA UJENZI
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
Sekta ya ujenzi nchini inaendelea kushuhudia mafanikio makubwa kutokana na mchango wa taasisi mbalimbali za Serikali zinazotekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Taasisi ya Ujenzi Tanzania (TBA), ambayo imeendelea kujidhihirisha kama nguzo muhimu katika kuhakikisha miradi ya Serikali inatekelezwa kwa ubora, usalama na kwa gharama zinazozingatia thamani halisi ya fedha za umma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonge, amepongeza kwa dhati utendaji wa TBA akieleza kuwa taasisi hiyo imekuwa mfano wa kuigwa katika sekta ya ujenzi kwa namna ilivyosaidia Serikali kupunguza gharama za ujenzi huku ikihakikisha majengo yanayojengwa yanakuwa salama, imara na yenye viwango vinavyokubalika.
Dkt. Msonge alitoa kauli hiyo alipokuwa akitembelea banda la TBA katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma. Alisema tangu kuanzishwa kwake, TBA imeendelea kutekeleza dhamira iliyokusudiwa kwa mafanikio makubwa na kuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.
Akizungumza mbele ya viongozi na wananchi waliotembelea maonesho hayo, Dkt.Msonge alisema Serikali inaiona TBA kama taasisi yenye mchango mkubwa katika kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayozingatia ubora, usalama na uwajibikaji.
“Mimi nitawashukuru na kuwapongeza sana TBA, mnafanya kazi nzuri sana. Katika taifa letu, taasisi hii ilivyoanzishwa ililenga kupunguza gharama za Serikali, lakini pia kuhakikisha usalama wa majengo na usimamizi wake unafanywa na taasisi ya Serikali,” alisema Dkt. Msonge huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza kasi hiyo ya utendaji.
Alifafanua kuwa mafanikio ya TBA yamechangiwa na uwezo wake wa kusimamia miradi kwa weledi, jambo ambalo limeiwezesha Serikali kuokoa fedha nyingi ambazo zinaweza kuelekezwa katika utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.
Kutokana na umuhimu huo, Dkt. Msonge alisema Serikali imeendelea kufanya maboresho ya sheria na kanuni ili kuipa TBA mamlaka na nafasi kubwa zaidi ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, sambamba na kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka katika sekta ya ujenzi.
Alisema maboresho hayo pia yatafungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya TBA na sekta binafsi, hatua ambayo itarahisisha uwekezaji katika ujenzi na upanuzi wa majengo ya Serikali pamoja na miundombinu mingine inayotoa huduma muhimu kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Dkt. Msonge, ushirikiano huo utaleta tija kubwa kwa kuongeza fursa za uwekezaji, kuimarisha matumizi bora ya rasilimali zilizopo na kuhakikisha Serikali inaendelea kupata thamani halisi ya fedha katika kila mradi unaotekelezwa, huku huduma kwa wananchi zikiendelea kuboreshwa.
Akihitimisha, Dkt. Msonge aliitaka TBA kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na uadilifu, huku ikitumia kikamilifu fursa zinazotokana na maboresho ya sheria na sera.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya kisera na kisheria yatakayoiwezesha taasisi hiyo kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuharakisha maendeleo ya sekta ya ujenzi na miundombinu nchini

