KILIMO MHIMILI IMARA WA MAWNDELEO YA VIWANDA
![]() |
| Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis L. Londo akizungumza na waandishi WA habari Dodoma |
Sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zimeendelea kupewa nafasi ya kipekee katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda kutokana na mchango wake mkubwa katika uzalishaji wa malighafi, ajira na biashara. Serikali inaamini kuwa kuongeza thamani ya mazao yanayotokana na sekta hizo kutafungua fursa mpya za uwekezaji, kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis L. Londo, amesema mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ndiyo msingi wa maendeleo ya viwanda na biashara nchini, huku akisisitiza kuwa kuongeza thamani ya mazao hayo ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane, Londo alisema mazao yanayozalishwa na wakulima, wafugaji na wavuvi hayapaswi kuonekana kama bidhaa za matumizi ya kawaida pekee, bali ni malighafi muhimu inayowezesha viwanda kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuongeza ushindani wa uchumi wa Taifa.
Alieleza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mazao hayo yanaongezewa thamani kabla ya kuingia sokoni, hatua ambayo itachochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira na kuinua kipato cha wazalishaji.
Londo alisema ushirikiano huo pia unalenga kuwajengea uwezo wazalishaji kutumia teknolojia za kisasa katika uchakataji wa mazao ili bidhaa zinazozalishwa zikidhi viwango vya ubora vinavyokubalika katika masoko ya ndani na kimataifa.
Aidha, alisema taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara zinashiriki katika Maonesho ya Nanenane kupitia banda namba tatu, zikiwemo BRELA, TBS, Tume ya Ushindani (FCC), SIDO pamoja na taasisi nyingine zinazotoa huduma mbalimbali kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
Alifafanua kuwa taasisi hizo zina jukumu muhimu la kurahisisha usajili wa biashara, kusimamia viwango vya ubora wa bidhaa, kuendeleza viwanda vidogo na vya kati pamoja na kuhakikisha ushindani wa haki katika shughuli za biashara nchini.
Kwa mujibu wa Londo, uwepo wa taasisi hizo katika maonesho hayo unatoa fursa kwa wananchi kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na namna zinavyoweza kuwasaidia kuongeza thamani ya bidhaa zao na kupanua masoko.
Akijibu swali kuhusu matarajio ya wakulima kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, alisema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya uzalishaji kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu mbalimbali.
Alisema Serikali imeendelea kujenga na kuboresha barabara, madaraja, vivuko, huduma za umeme kupitia REA pamoja na miundombinu ya mawasiliano, hatua ambazo zimepunguza changamoto za uzalishaji na usafirishaji wa mazao kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Londo aliongeza kuwa maboresho hayo yanawawezesha wazalishaji kufikia masoko kwa urahisi zaidi, kupata taarifa za bei na fursa za biashara kwa wakati kupitia mifumo ya mawasiliano, jambo linaloongeza tija na ushindani wa bidhaa zao.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kuhamasisha ongezeko la thamani katika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili sekta hizo ziendelee kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya viwanda, ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

