TABIO Yatoa Wito wa Kupunguza Utegemezi wa Kemikali Kilimoni
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
WAKULIMA nchini wamehimizwa kuachana na utegemezi mkubwa wa pembejeo za kemikali na kuelekea katika matumizi ya pembejeo za kilimo ikolojia hai, hatua inayotajwa kuwa suluhisho la uzalishaji endelevu, usalama wa chakula na ulinzi wa afya za walaji pamoja na mazingira. Wataalamu wanasema mabadiliko hayo si tu yataongeza tija ya uzalishaji wa mazao, bali pia yatarejesha rutuba ya udongo, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuweka msingi imara wa kilimo chenye manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO), Abdallah Mkindi, wakati wa mdahalo kuhusu pembejeo za kilimo ikolojia hai uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo kwenye Maonesho ya Nanenane, ulioandaliwa na TABIO, ambapo wadau wa sekta ya kilimo walikutana kujadili nafasi ya pembejeo za asili katika kuimarisha uzalishaji endelevu na usalama wa chakula nchini.
Mkindi amesema kilimo ikolojia hai ni mfumo unaoweka uwiano kati ya uzalishaji, afya ya binadamu na utunzaji wa mazingira, akieleza kuwa matumizi ya pembejeo za asili yanatoa fursa ya kuongeza uzalishaji bila kuathiri ubora wa udongo wala afya ya walaji.
Amesema matumizi makubwa na yasiyo sahihi ya kemikali za kilimo yameendelea kuzua hofu kutokana na tafiti mbalimbali kuonyesha kuwa yanaweza kuongeza hatari ya magonjwa mbalimbali, ikiwemo baadhi ya aina za saratani, sambamba na kuchafua udongo na vyanzo vya maji vinavyotegemewa na jamii.
"Hii ndiyo sababu tunaendelea kuwajengea uwezo wakulima kutumia mbinu rafiki kwa mazingira. Tunataka mkulima azalishe chakula salama, alinde afya yake, familia yake na mlaji kwa ujumla huku akihifadhi rutuba ya ardhi kwa vizazi vijavyo," amesema Mkindi.
Katika mdahalo huo, Mwija Irika kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania alisema Sheria ya Mbolea imefungua fursa mbalimbali kwa wawekezaji na wazalishaji wa mbolea za asili, huku taratibu za usajili zikiwa wazi na rafiki kwa wawekezaji. Amesema hadi sasa zaidi ya aina 65 za mbolea za asili zimesajiliwa nchini, huku wazalishaji 15 wakiwa tayari wanafanya shughuli za uzalishaji.
Irika amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta hiyo pamoja na kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea za asili, akibainisha kuwa matumizi yake huchangia kuboresha rutuba ya udongo kwa muda mrefu, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza uzalishaji wa mazao salama kwa walaji.
Naye Senior Program Coordinator wa CSWED Tanzania, Gladness Martini, amesema tafiti shirikishi zimekuwa na mchango mkubwa katika kuwasaidia wakulima kutambua, kuzalisha na kuhifadhi mbegu za asili zenye ubora. Amesema ushirikishwaji wa wakulima katika hatua zote za utafiti huwajengea uwezo wa kuelewa nafasi yao katika maendeleo ya teknolojia za kilimo na kunufaika moja kwa moja na matokeo yake.
Martini ameongeza kuwa mbegu za asili zinazofanyiwa utafiti na kuthibitishwa kisayansi zina uwezo wa kuongeza uzalishaji huku zikiendana na mazingira ya maeneo husika, jambo linalochangia kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wakulima na kukuza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.
Kwa upande wake, mkulima mtafiti Julina David amesema pamoja na jitihada hizo, wakulima wengi bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo za asili, hususan viuatilifu, pamoja na kuelekezwa kwa ruzuku nyingi kwenye pembejeo za viwandani.
Amesisitiza umuhimu wa kuwajengea wananchi uwezo wa kutengeneza mbolea na viuatilifu vya asili kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yao, akieleza kuwa elimu ndiyo msingi wa mafanikio ya kilimo ikolojia hai na kwamba mifumo ya uzalishaji inapaswa kulinda mazingira ili kuhakikisha teknolojia hizo zinakuwa endelevu.
Naye mdau wa kilimo, Ismail Shaban, amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza elimu kwa wakulima kuhusu faida za mbolea za asili na namna sahihi ya kuzitumia. Amesema uelewa mdogo kuhusu uwezo wa pembejeo hizo kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za kilimo na kuhifadhi afya ya udongo umeendelea kuwa sababu inayochangia matumizi yake kuwa madogo, hivyo akatoa wito kwa Serikali, taasisi za utafiti na wadau wa maendeleo kuimarisha utoaji wa elimu ili kuharakisha mpito kuelekea kilimo endelevu nchini.

