Breaking News

UVIDA Yatajwa Kuwa Tishio Kubwa; FAO Yasisitiza Ufugaji Bora Kulinda Afya na Usalama wa Chakula

 


Na. Wellu Mtaki, Dodoma 

Matumizi yasiyo sahihi ya dawa katika sekta ya mifugo na kilimo yameendelea kuzua hofu kutokana na kuongezeka kwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa (UVIDA), hali inayotajwa kuhatarisha afya ya binadamu na usalama wa chakula. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linasema suluhisho la changamoto hiyo linaanzia kwenye kuzingatia mbinu bora za ufugaji na matumizi sahihi ya dawa.

Akizungumza leo katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mtaalamu wa Udhibiti wa Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa kutoka FAO, Dkt. Elibariki Mwakapeje, alisema UVIDA imeendelea kuwa moja ya changamoto kubwa duniani, huku ikisababisha vifo vingi vinavyozidi hata baadhi ya magonjwa makubwa kama malaria, UKIMWI na kifua kikuu (TB).

Alieleza kuwa matumizi holela ya dawa kwa mifugo na mazao yanachangia kuibuka kwa vimelea vinavyoshindwa kutibika kwa urahisi, jambo linaloongeza hatari ya maambukizi kwa binadamu na kuifanya tiba kuwa ngumu na ya gharama kubwa zaidi.

Dkt. Mwakapeje aliwataka wakulima na wafugaji kuzingatia kanuni bora za ufugaji ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya dawa, akisisitiza kuwa kinga kupitia usimamizi mzuri wa mifugo ni njia bora kuliko kutegemea matibabu ya mara kwa mara.

Alisema FAO imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kuimarisha usalama wa chakula nchini, ikiwemo kufanya uchunguzi wa ubora wa maziwa katika maeneo ya wafugaji wa Kimasai na Simanjiro, ambapo matokeo yalionesha uwepo wa kiwango kikubwa cha vimelea.

Kutokana na matokeo hayo, alisema shirika hilo lilitoa elimu kwa wafugaji kuhusu mbinu bora za ufugaji, usafi wa mazingira na uzalishaji wa maziwa salama ili kulinda afya ya walaji na kuongeza ubora wa bidhaa za mifugo.

Aidha, FAO imeendesha mafunzo ya ufugaji bora wa kuku yaliyolenga kupunguza matumizi holela ya dawa, ambapo baadhi ya wafugaji wamefanikiwa kufuga kuku bila kutumia dawa kutokana na kufuata taratibu sahihi za ufugaji na usimamizi wa afya ya mifugo.

Kwa mujibu wa Dkt. Mwakapeje, mafunzo hayo yamefanyika katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Ilala na Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Kihonda na Bigwa mkoani Morogoro, pamoja na Arusha, ambapo jumla ya wafugaji 185 walihitimu na kutunukiwa vyeti.

Alisema wahitimu hao wameendelea kuwa mabalozi wa elimu katika jamii zao, hatua iliyowezesha zaidi ya wafugaji 2,000 nchini kuanza kufuga kuku wa kisasa kwa kuzingatia mbinu bora zinazowapunguzia utegemezi wa matumizi ya dawa.

Akihitimisha, Dkt. Mwakapeje alisema mafanikio hayo yanatokana na kuhamasisha ujenzi wa mabanda yenye uingizaji mzuri wa hewa, yanayozuia wadudu kuingia, pamoja na kuzingatia usafi wa mazingira na taratibu za kujitakasa kwa maafisa ugani au wageni kabla ya kuingia katika shamba jingine, ili kuzuia kusambaza vimelea kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kulinda afya ya mifugo pamoja na binadamu.