Breaking News

Serikali Yaongeza Kasi Maendeleo Kasulu

 


Na Wellu Mtaki, Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Edibily Kazala Kinyoma, amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji, elimu pamoja na huduma za afya.

Kazala ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuahirishwa kwa Bunge, ambapo ameeleza kuwa hali ya barabara katika maeneo mbalimbali ya Kasulu imeendelea kuboreshwa.

Amesema kuwa baadhi ya barabara ambazo awali zilikuwa hazipitiki, hasa wakati wa mvua, sasa zimeanza kupitika kutokana na juhudi za Serikali katika kuzifanyia matengenezo na kuziboresha.

“Serikali inaendelea kufanya kazi, hasa katika upande wa barabara. Hapo awali kulikuwa na barabara ambazo hazipitiki, lakini sasa zimeanza kupitika. Katika maeneo mengine wakandarasi wapo site na wanaendelea na kazi za matengenezo,” amesema Kazala.

Aidha, amesema bajeti ya utekelezaji wa miradi mbalimbali imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 2.2 hadi kufikia Shilingi bilioni 2.3, huku upande wa maji ukitengewa Shilingi bilioni 1.5 ambazo, kwa kuanzia zitasaidia kusogeza huduma hiyo kwa wananchi.

Kwa upande wa elimu, Kazala amesema Serikali inaendelea na mipango ya kutekeleza ahadi zilizotolewa kwa wananchi, ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari za kidato cha tano na sita katika maeneo yaliyolengwa.

Amesema wananchi wanapaswa kuwa na matumaini na kuendelea kusubiri utekelezaji wa ahadi hizo, huku akieleza kuwa huduma za afya nazo zimepewa kipaumbele, hususan katika maeneo ya Kasulu vijijini na maeneo mengine ya jimbo hilo.

Katika hatua nyingine, Kazala amesisitiza umuhimu wa viongozi kutambua kuwa madaraka ni dhamana wanayopewa na wananchi, hivyo kiongozi anayeshindwa kutekeleza wajibu wake anapaswa kuwa tayari kupisha nafasi hiyo.

“Kiongozi yupo kwa niaba ya wananchi. Kama kiongozi ameona hayupo katika nafasi hiyo kwa lengo la kukidhi matakwa ya wananchi, basi anapaswa kupisha nafasi hiyo ili mwananchi mwingine mwenye sifa na uwezo wa kuongoza aweze kupewa nafasi,” amesema.

Ameongeza kuwa kushikilia madaraka wakati kiongozi hawezi kutekeleza wajibu aliopewa hakupaswi kuonekana kama jambo la kawaida, kwa kuwa nafasi ya uongozi ni ya kuwahudumia wananchi na si mali ya mtu binafsi.

Kazala amesema kauli hiyo haipaswi kutafsiriwa kama tamaa ya madaraka, bali ni sehemu ya uwajibikaji na kuhakikisha wananchi wanapata viongozi wenye uwezo, uadilifu na utayari wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amesema lengo kubwa ni kuhakikisha maendeleo yanaendelea kupatikana katika maeneo mbalimbali ya Kasulu na kwamba Serikali, viongozi pamoja na wananchi wanapaswa kushirikiana katika kusukuma mbele maendeleo ya jimbo hilo