Breaking News

KALALA AMPONGEZA SAMIA KWA UTEUZI

Na. Wellu Mtaki, Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Edibily Kazala Kinyoma, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uteuzi wa kijana kuwa Makamu wa Rais,  akisema hatua hiyo ni ishara ya wazi ya imani na matumaini kwa vijana wa Kitanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge mara baada ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge, Mbunge Kazala amesema uteuzi huo umeonyesha namna Serikali inavyotambua nafasi, uwezo na nguvu ya vijana katika kuleta mabadiliko na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Amesema vijana ni sehemu kubwa ya nguvu kazi ya Taifa, huku akieleza kuwa takribani asilimia 60 ya Watanzania ni vijana. Kwa mujibu wake, kundi hilo lina nguvu, ubunifu, mawazo mapya na uwezo mkubwa wa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo iwapo litawezeshwa na kuaminiwa.

“Fahari ya vijana ni nguvu yao,” amesema Mbunge Kazala, akinukuu maandiko matakatifu na kusisitiza kuwa nguvu, uthubutu na ubunifu wa vijana vinapaswa kutumika katika kujenga Taifa lenye uchumi imara na maendeleo endelevu.

Amesema uamuzi wa kumteua kijana katika nafasi hiyo ya juu umeigusa mioyo ya vijana wengi nchini, kwani unawapa matumaini kwamba wanaweza kuaminiwa na kupewa nafasi katika uongozi wa Taifa.

Mbunge huyo amesisitiza kuwa hatua hiyo ni zaidi ya uteuzi wa mtu mmoja, bali ni ujumbe mpana kwa vijana wote kwamba wana nafasi kubwa katika ujenzi wa Tanzania ya sasa na ya baadaye.

Aidha, Kazala ametoa pongezi kwa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa hatua hiyo, akieleza kuwa ni sehemu ya mwelekeo wa chama katika kuwapa vijana nafasi na kuwaandaa kushiriki kikamilifu katika uongozi na maendeleo ya Taifa.

Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kuendelea kujenga uwezo, kutumia fursa zinazopatikana na kuwa tayari kuchukua majukumu makubwa pale wanapoaminiwa, kwa sababu Tanzania yenye maendeleo inahitaji nguvu, mawazo na ushiriki wa vijana.

ikumbukwe kuwa Chama Tawala nchini Tanzania CCM kimepitisha Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi kuchukua nafasi ya Makamu wa Rais wa Tanzani.