Breaking News

TPHPA yaokoa mazao ya chakula zaidi ya tani milioni 1.4, yafungua masoko mapya ya kimataifa

 

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph C. Ndunguru, Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Agosti 27, 2026.

Na. Wellu Mtaki Dodoma

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeeleza kuwa hatua mbalimbali ilizochukua katika mwaka wa fedha 2025/2026 zimewezesha kulinda mazao ya chakula, kudhibiti visumbufu na magonjwa ya mimea, pamoja na kufungua fursa mpya za biashara ya mazao ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Agosti 27, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph C. Ndunguru, alisema mafanikio hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha nchi inakuwa na usalama na utoshelevu wa chakula huku wakulima wakipata masoko yenye tija kwa mazao yao.

Kwa mujibu wa Prof. Ndunguru, Tanzania ilifikia kiwango cha utoshelevu wa chakula cha asilimia 130 katika mwaka huo, huku uzalishaji wa chakula ukifikia tani 23,783,128.

 Alisema TPHPA ilichangia mafanikio hayo kwa kudhibiti visumbufu na magonjwa ya mimea ambavyo vina uwezo wa kusababisha hasara kubwa kwa wakulima na kupunguza uzalishaji.

Miongoni mwa mafanikio makubwa ni udhibiti wa kwelea kwelea, ambapo ndege hao milioni 233.5 waliovamia wilaya 21 walidhibitiwa kwa njia ya anga kwa kutumia ndege na ndege nyuki.

 Hatua hiyo, alisema, iliokoa takribani tani 1,092,780 za mazao ya nafaka, yakiwemo mtama, uwele na mpunga, ambazo zingepotea kutokana na mashambulizi ya ndege hao.

Katika mapambano dhidi ya viwavijeshi, TPHPA ilitekeleza operesheni katika halmashauri 52 zilizoathirika, huku lita 54,846 za viuatilifu zikitumika kudhibiti wadudu hao katika mashamba yenye ukubwa wa ekari 228,525. Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, hatua hiyo iliwezesha kuokoa takribani tani 342,787.5 za mazao ya nafaka.

Baa la panya nalo lilikuwa miongoni mwa changamoto zilizoshughulikiwa, ambapo TPHPA ilifanya udhibiti katika mikoa sita, wilaya 13, kata 392 na vijiji 14,122, na kufanikiwa kuokoa ekari 73,136 za mazao. Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kulinda uzalishaji wa chakula mashambani.

TPHPA pia imeanza kutegemea zaidi sayansi na teknolojia katika kutambua visumbufu na magonjwa ya mimea. Katika Wilaya ya Mpwapwa, kwa mfano, wataalamu walitumia teknolojia ya PCR na DNA Sequencing kuchunguza nzige waliodhaniwa kuwa nzige wekundu, lakini uchunguzi ulibaini kuwa walikuwa aina ya Tree Locust – Anacridium incisum, huku uchambuzi wa BLAST ukionyesha ufanano wa asilimia 96.52.

Teknolojia hiyo pia imetumika katika uchunguzi wa magonjwa ya mimea, ikiwamo katika Wilaya ya Kilolo, ambako sampuli za mazao ya mbogamboga zilichunguzwa kwa kutumia DNA sequencing. Matokeo yaliwasaidia wataalamu kuwaelimisha wakulima kuhusu vimelea vilivyobainika na kuwaandalia mikakati ya kudhibiti magonjwa hayo kwa njia endelevu.

Katika upande wa biashara ya mazao, TPHPA imeeleza kuwa kampuni nane mpya za Tanzania ziliruhusiwa kusafirisha parachichi kwenda China baada ya kutimiza matakwa ya soko hilo. Hatua hiyo imefanya jumla ya kampuni za Tanzania zilizoidhinishwa kusafirisha parachichi nchini China kufikia 24, jambo linalotarajiwa kuongeza fursa kwa wakulima, vijana na wadau wa kilimo biashara.

Mbali na parachichi, TPHPA kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau wengine iliwezesha usajili wa kampuni 444 za Tanzania katika mfumo wa forodha wa China (GACC), hatua inayofungua milango kwa biashara ya mazao mbalimbali. Aidha, kampuni tano za ufukiziaji maalumu kwa mazao yanayopelekwa China zilisajiliwa ili kuimarisha uzingatiaji wa viwango vya soko hilo.

Mamlaka hiyo pia imefungua soko la Seychelles kwa mazao 10 hadi kufikia Juni 2026, yakiwemo kabichi, parachichi aina ya Hass, maharage mabichi, karoti, viazi, kitunguu saumu, tangawizi, kitunguu maji, nanasi na mimea ya viungo pamoja na viungo lishe. Kwa upande mwingine, TPHPA imeendelea kulinda masoko yaliyopo kwa kuhakikisha mazao ya Tanzania yanaendelea kukidhi viwango vya nchi zinazoagiza.

Mfano wa hatua hizo ni uchunguzi uliofanywa kuhakikisha Tanzania inakidhi matakwa ya Umoja wa Ulaya kuhusu bakteria aina ya Xylella fastidiosa. TPHPA ilichukua sampuli 5,664 za mazao mbalimbali na kufanya uchunguzi kwa kutumia PCR, ambapo matokeo yalionyesha Tanzania haina bakteria huyo, hivyo kuendelea kulinda uaminifu wa mazao ya Tanzania katika soko la Umoja wa Ulaya.

TPHPA, iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Afya ya Mimea, Sura ya 133 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake Februari 1, 2021, kwa sasa inatekeleza majukumu kupitia Makao Makuu ya Arusha, Kanda saba Tanzania Bara na vituo 47 rasmi vya ukaguzi katika mipaka ya nchi kavu, bandari na viwanja vya ndege. Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, mamlaka hiyo inalenga kuendeleza udhibiti wa visumbufu, kuimarisha matumizi ya teknolojia, usalama wa viuatilifu, uhifadhi wa bioanuwai na ufunguaji pamoja na ulinzi wa masoko ya kimataifa kwa mazao ya Tanzania.