PBA Yapanua Huduma Nanenane
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
Wananchi wanaotembelea maonesho ya Nanenane mwaka huu wamepata fursa ya kupata huduma za msaada wa kisheria, huku Chama cha Mawakili wa Serikali nchini (PBA) kikihakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Rais wa PBA, Wakili Bonifeniture Mwambaja, amesema hayo leo mkoani Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya 49 ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Malecela.
Amesema PBA imejipanga kutumia maonesho hayo kuwa sehemu ya kuwafikia wananchi wenye changamoto za kisheria na kuwapatia ushauri pamoja na msaada unaohitajika bila kujali wanatoka mkoa gani.
Kwa mujibu wa Mwambaja, mpango huo hauishii Dodoma pekee, bali umeandaliwa kwa lengo la kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinapatikana katika mikoa mbalimbali nchini ili wananchi waweze kupata suluhisho la changamoto zao.
Amesema katika ziara yake kwenye mabanda ya PBA kutoka mikoa mbalimbali, amejionea namna mawakili wa serikali walivyojiandaa kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto zinazohusu masuala ya sheria.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana Dodoma, Mwambaja ameipongeza timu ya mkoa huo kwa kazi iliyofanyika, akisema tayari imefanikiwa kuwahudumia wananchi 98 wenye mahitaji ya msaada wa kisheria.
Amesema idadi hiyo imefikiwa kupitia huduma zinazotolewa kila siku, ambapo wastani wa wananchi 10 hadi 12 hupata msaada wa kisheria katika banda la PBA mkoani Dodoma.
Mwambaja amezitaka timu za PBA katika mikoa mingine kutumia uzoefu wa Dodoma kama mfano wa namna bora ya kuwafikia wananchi na kusaidia kutatua changamoto zao katika nyanja mbalimbali za sheria.
Amesema mwitikio wa wananchi umeonyesha umuhimu wa huduma hiyo, akibainisha kuwa baadhi ya wanaofika katika banda la PBA Dodoma wanatoka hata mikoa jirani kwa ajili ya kupata ushauri na msaada wa kisheria.
“Ni jambo la kuwapongeza kuona watu wametoka katika mikoa ya jirani na wamekuja hapa kupata huduma,” amesema Mwambaja, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha huduma hiyo kwa manufaa ya wananchi


