TEKNILOJIA CHACHU YA KILIMO
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
Wakati Tanzania ikilenga kuongeza tija katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, Serikali imeelekeza nguvu katika matumizi ya maarifa, taarifa sahihi na teknolojia za kisasa, ikiamini kuwa hatua hiyo inaweza kufungua milango mipya ya uzalishaji wenye tija na ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, ambapo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara amesema maarifa na taarifa sahihi ni nguzo muhimu katika kuongeza uzalishaji na kufanikisha malengo yaliyowekwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema Serikali inalenga kuona mazao yanayotokana na kilimo, mifugo na uvuvi hayauzwi kwa mfumo wa kawaida pekee, bali yanaongezewa thamani kupitia uwekezaji katika viwanda na usindikaji, hatua ambayo itasaidia kuongeza kipato cha wananchi, kuibua ajira na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.
Katika kuhakikisha uzalishaji unakuwa na tija zaidi, Serikali pia imeeleza kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya uzalishaji kwa kuimarisha miundombinu ya barabara kupitia TARURA, kuwezesha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na kuendelea kutoa ruzuku kwa lengo la kupunguza gharama zinazowakabili wakulima.
Hatua hizo zinaelezwa kuwa sehemu ya jitihada pana za kuufanya uzalishaji wa ndani kuwa msingi wa uchumi shindani, huku wakulima, wafugaji na wavuvi wakihimizwa kutumia fursa zinazotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika kuboresha shughuli zao za kila siku.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo kwa Utaratibu wa Koroba nchini, Geoffrey Kilenga, amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na mahitaji ya bidhaa katika masoko ya Afrika Mashariki, SADC, Ulaya, Asia na Marekani.
Hata hivyo, Kilenga amesema kufunguka kwa masoko hayo pekee hakutoshi, kwani mafanikio ya Tanzania yanategemea uwezo wa kuzalisha mazao yenye ubora, usalama na viwango vinavyokubalika katika masoko ya kimataifa.
Amesema mkutano huo umeibua kwa namna ya pekee umuhimu wa kutumia sayansi na teknolojia katika kuthibitisha ubora wa mazao, hususan nafaka ambazo zinaweza kuathiriwa na sumukuvu inayojulikana kama aflatoxin.
Miongoni mwa teknolojia zilizopewa uzito ni kifaa cha AflaBox, ambacho kina uwezo wa kusaidia kubaini kwa haraka uwepo wa sumukuvu kwenye nafaka bila kulazimika kupeleka sampuli katika maabara kwa ajili ya uchunguzi wa awali.
Kwa mujibu wa Kilenga, matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kuwapa wakulima, wasindikaji na wanunuzi uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu ubora wa mazao kabla hayajafikishwa sokoni, jambo litakalosaidia kupunguza hatari kwa afya ya walaji.
Aidha, amesema hatua hiyo inaweza kuongeza thamani na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa, kwa kuwa ubora na usalama wa chakula ni miongoni mwa vigezo muhimu vinavyoangaliwa na wanunuzi na nchi zinazoagiza bidhaa kutoka nje.
Ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanachagua mazao yanayotoka katika maeneo yanayozingatia viwango vya ubora, huku akiwasisitiza wakulima, wafugaji na wadau wengine kuendelea kufuata ushauri wa wataalamu ili kulinda usalama wa chakula, afya ya jamii na kujenga sekta ya uzalishaji yenye tija na ushindani.

