UDSM YAONGEZA THAMANI YA MAZAO YA NYUKI KUFUNGUA FURSA ZA AJIRA NA BIASHARA
Na Wellu Mtaki, Dodoma
Katika jitihada za kuimarisha matumizi ya teknolojia na utafiti katika sekta ya kilimo na ufugaji, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimekuja na ubunifu unaolenga kubadilisha mazao ya nyuki kuwa bidhaa mbalimbali zenye matumizi ya kila siku. Ubunifu huo unaweka msisitizo katika kuongeza thamani ya asali, nta na mazao mengine ya nyuki, huku ukilenga kuwasaidia wafugaji na wadau wengine kunufaika zaidi na sekta hiyo kupitia masoko mapya, ajira na fursa za ujasiriamali.
Akizungumza katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, mwanafunzi wa Ndaki ya Sayansi za Kilimo na Teknolojia ya UDSM, Josiana Donald, alisema chuo hicho kimekuwa kikifanya tafiti na ubunifu mbalimbali katika ufugaji wa nyuki wakubwa na nyuki wadogo.
Donald alisema tafiti hizo hazilengi tu kuongeza uzalishaji wa asali, bali pia kutafuta njia za kutumia mazao ya nyuki kutengeneza bidhaa zinazoweza kutumika katika maisha ya kila siku na kuwa na thamani kubwa zaidi sokoni.
“UDSM tunafanya ufugaji wa nyuki wakubwa pamoja na nyuki wadogo. Kupitia tafiti tunazofanya, tumeweza kubaini namna mazao yao yanavyoweza kutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zinaweza kuwa na manufaa kwa jamii na pia kutoa fursa za kiuchumi,” alisema.
Alisema miongoni mwa bidhaa ambazo UDSM imefanikiwa kuzalisha ni asali ya nyuki wakubwa na nyuki wadogo, dawa ya kikohozi, dawa ya kung’arisha viatu inayojulikana kama Royal Spray Shoe Polish, shower gel pamoja na sabuni za mikono.
Kwa mujibu wa Donald, dawa ya kikohozi ni miongoni mwa bidhaa zilizotengenezwa kwa kuzingatia matumizi ya asali ya nyuki wadogo, ambayo huchanganywa na tangawizi pamoja na viambato vingine vya tiba asili.
Alisema bidhaa hiyo inalenga kusaidia kupunguza changamoto mbalimbali zinazohusiana na kikohozi na mafua, huku ikionesha namna ambavyo mazao ya nyuki yanaweza kutumika zaidi ya matumizi ya kawaida ya asali kama chakula.
“Tumetengeneza pia dawa ya kikohozi kwa kutumia asali ya nyuki wadogo pamoja na tangawizi na viambato vingine vya tiba asili. Hii inaonesha kwamba mazao ya nyuki yanaweza kutumika kutengeneza bidhaa zenye matumizi tofauti,” alisema.
Aidha, Donald alisema UDSM imefanya ubunifu katika matumizi ya nta ya nyuki wakubwa kwa kutengeneza dawa ya kung’arisha viatu, Royal Spray Shoe Polish.
Alisema bidhaa hiyo inasaidia kufanya viatu kuwa na mwonekano mzuri na kuongeza thamani ya matumizi ya nta ambayo wakati mwingine inaweza kuuzwa kama malighafi bila kuchakatwa zaidi.
Mbali na bidhaa hizo, alisema chuo hicho pia kinazalisha shower gel na sabuni za mikono zinazotumia asali kama mojawapo ya malighafi.
Kwa mujibu wa Donald, bidhaa hizo zina manufaa katika utunzaji wa ngozi kwa kusaidia kuongeza unyevunyevu na kuifanya ngozi kuwa katika hali nzuri, huku zikiwa sehemu ya jitihada za kutumia malighafi zinazopatikana kutoka kwenye mazao ya nyuki.
Alisema ubunifu huo umejengwa kutokana na changamoto inayowakabili baadhi ya wafugaji wa nyuki ambao mara nyingi huuza asali, nta na mazao mengine ya nyuki yakiwa katika hali ghafi
Hali hiyo, alisema, inaweza kuwafanya wafugaji kupata kipato kidogo ikilinganishwa na faida inayoweza kupatikana endapo mazao hayo yatachakatwa na kugeuzwa kuwa bidhaa zenye thamani zaidi.
“Changamoto kubwa ni kwamba wafugaji wengi wanauza mazao ya nyuki bila kuyaongezea thamani. Tukiyaongezea thamani, tunafungua masoko mapya na mfugaji anaweza kupata kipato zaidi,” alisema.
Alifafanua kuwa uwekezaji katika uchakataji wa mazao ya nyuki unaweza pia kuibua shughuli nyingine za kiuchumi katika mnyororo wa thamani, ikiwemo uzalishaji, ufungashaji, usafirishaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa.
Donald alisema utafiti na ubunifu unaofanywa na UDSM ni sehemu ya jitihada za kuonesha namna elimu inayopatikana katika taasisi za elimu ya juu inaweza kutumika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na wakati huo huo kuibua fursa za kiuchumi.
Alisema sekta ya ufugaji nyuki ina nafasi kubwa katika kukuza kipato cha wananchi iwapo itasimamiwa kwa kutumia maarifa, teknolojia na ubunifu unaoweza kuongeza tija na thamani ya mazao.
Aidha, aliwataka wafugaji, vijana, wanawake, wawekezaji na wananchi kwa ujumla kutumia fursa zinazopatikana katika sekta ya nyuki kwa kujifunza namna ya kuzalisha na kuchakata mazao yake.
Aliwahimiza wadau mbalimbali kutembelea banda la UDSM katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma ili kupata elimu kuhusu teknolojia za ufugaji wa nyuki, tafiti zinazofanywa na chuo hicho pamoja na bidhaa zinazoweza kuzalishwa kutokana na mazao ya nyuki.
Alisema ushirikiano kati ya watafiti, wafugaji, wawekezaji na jamii ni muhimu katika kuhakikisha ubunifu unaofanywa katika taasisi za elimu unafika kwa wananchi na kutumika kuongeza uzalishaji, kipato na ajira.
Kwa ujumla, ubunifu huo wa UDSM unaonesha kuwa ufugaji nyuki hauishii katika uzalishaji na uuzaji wa asali pekee, bali una nafasi ya kuanzisha mnyororo mpana wa bidhaa na huduma. Kwa kuongeza thamani ya mazao ya nyuki kupitia utafiti na teknolojia, wafugaji na wajasiriamali wanaweza kupata fursa ya kufikia masoko mapya na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa jamii.
