Breaking News

TOSCI: Mbegu Bora Zafungua Fursa za Kilimo Biashara na Masoko ya Kimataifa

 


Na Hawa Ismail, Dar es Salaam

Matumizi ya mbegu bora yameendelea kutajwa kuwa msingi wa mafanikio ya kilimo biashara nchini, huku yakitajwa kuongeza uzalishaji wenye tija, kuimarisha usalama wa chakula na kufungua fursa za wakulima na wawekezaji kunufaika na masoko ya ndani na kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Nyasebwa Chimagu, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhimiza kilimo biashara, ambapo matumizi ya mbegu bora ndiyo msingi wa kuongeza tija na ushindani wa mazao ya Tanzania.

"Serikali imeendelea kusisitiza kilimo biashara, na msingi wa kilimo biashara ni matumizi ya mbegu bora. Sisi kama TOSCI jukumu letu ni kuhakikisha mbegu zote zinazowafikia wakulima zimehakikiwa na kuthibitishwa ubora wake," alisema Chimagu.

Alieleza kuwa TOSCI ina jukumu la kusajili aina mpya za mbegu baada ya kupitia majaribio yanayothibitisha ubora wake, uwezo wa kustawi katika mazingira mbalimbali ya Tanzania pamoja na sifa zake za uzalishaji. Aidha, taasisi hiyo husajili wazalishaji wa mbegu na mashamba ya uzalishaji huku ikifanya ukaguzi katika kila hatua ili kuhakikisha mbegu zinakidhi viwango vya ubora.

"Tunafanya ukaguzi kuanzia shambani hadi maabara ili kuhakikisha mbegu zote zinakidhi viwango vya ubora. Tunachukua sampuli na kufanya uchunguzi kuhakikisha mbegu hizo zina sifa zilizosajiliwa," alisema.

Chimagu alisema TOSCI pia imeanzisha mfumo wa kidijitali unaowezesha wakulima kuhakiki uhalali wa mbegu kabla ya kuzinunua. Alifafanua kuwa mbegu halali lazima ziwe zimefungashwa na kuwa na lebo maalumu ya TOSCI, akisisitiza kuwa ni kinyume cha sheria kuuza mbegu ambazo hazijafungashwa.

"Mbegu zote zinazouzwa lazima ziwe kwenye kifungashio. Ni marufuku kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu kuuza mbegu ambazo hazijafungashwa kwa sababu kifungashio kina taarifa zote muhimu za mbegu pamoja na lebo ya uthibitisho wa TOSCI," alisema.

Aliongeza kuwa mkulima anaweza kuhakiki ubora wa mbegu kwa kutumia simu ya mkononi kupitia mfumo wa 14852#, ambapo akiingiza namba iliyopo kwenye lebo hupata taarifa zinazoonesha kama mbegu hiyo ni halisi au la.

"Ukipata taarifa kuwa mbegu ni halisi, ujue imepitia taratibu zote za uhakiki wa ubora. Ikiwa si halisi, tunawataka wananchi watoe taarifa mara moja ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika," alisisitiza.

Kwa mujibu wa Chimagu, Tanzania imejijengea uwezo mkubwa wa kuzalisha mbegu zinazokidhi viwango vya kimataifa kutokana na uwepo wa maabara ya taifa yenye ithibati ya kimataifa, hali inayowezesha mbegu zinazozalishwa nchini kuuzwa katika masoko mbalimbali ya nje.

"Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zenye maabara ya mbegu inayotambulika kimataifa. Hii inatupa fursa ya kuzalisha na kuuza mbegu zetu katika masoko ya kimataifa kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika duniani," alisema.

Alisema kupitia Maonesho ya Sabasaba, TOSCI inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mbegu bora, uzalishaji na biashara ya mbegu pamoja na fursa zilizopo katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Chimagu aliwahimiza wakulima, wawekezaji na wadau wa sekta ya kilimo kutembelea banda la TOSCI ili kupata elimu kuhusu teknolojia za uzalishaji wa mbegu bora na namna ya kushiriki katika biashara ya mbegu, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza tija katika kilimo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.