Breaking News

WAZIRI WA FEDHA: WAWEKEZAJI WAZAWA WABEBE SAFARI YA TANZANIA KUFIKIA UCHUMI WA DOLA TRILIONI MOJA

 


Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amewataka Watanzania kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi, akisisitiza kuwa wawekezaji wazawa wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa dola za Marekani trilioni moja.

Akizungumza jana katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Waziri Omar aliwahamasisha wananchi kutembelea banda la Wizara ya Fedha na taasisi zake ili kujionea huduma mbalimbali za kifedha pamoja na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.

Alisema uchumi wa Tanzania kwa sasa unakadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni 100, hivyo kuna wajibu wa kuuongeza mara kumi ili kufikia lengo la dola trilioni moja kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta za uzalishaji.

"Wakati mwingine tunafikiri uwekezaji mkubwa lazima ufanywe na wageni, lakini hata Watanzania wenye uwezo wanaweza kuwekeza na kuwa sehemu ya mabadiliko ya uchumi wetu. Tunataka wawekezaji wa ndani wawe mstari wa mbele," alisema Waziri Omar.

Alieleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuweka sera na mifumo rafiki, huku taasisi za kifedha zikiwa tayari kutoa mitaji na huduma mbalimbali kwa wananchi wanaotaka kuanzisha au kupanua biashara na miradi ya maendeleo.

Aidha, alisema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 umeanza kupitia Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, unaotekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi wa reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na kutoka Tanga kupitia Arusha hadi Musoma, pamoja na kuendelea kukamilisha sehemu zinazoendelea kujengwa.

Waziri Omar pia alisema Serikali inalenga kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka zaidi ya megawati 4,000 za sasa hadi kufikia megawati 8,000, sambamba na kuendelea kutekeleza miradi ya maji, umwagiliaji, barabara na mawasiliano ili kuongeza tija ya uchumi.

Alisisitiza kuwa miradi hiyo itafungua fursa zaidi za ajira, kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi wa taifa, huku sekta ya fedha ikiwa imejipanga kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika safari ya maendeleo.

Alihitimisha kwa kuwahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kufika katika banda la Wizara ya Fedha ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi zake pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana nchini.