TTCL yaongeza kasi ya ufanisi, yakabidhi magari sita ya Sh milioni 903 kuboresha huduma
Na Mwandishi Wetu
Katika kuimarisha utoaji wa huduma za mawasiliano nchini, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limekabidhi magari sita mapya yenye thamani ya Shilingi milioni 903 kwa viongozi wa idara za kiufundi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa usimamizi wa miundombinu na kuboresha huduma kwa wananchi.
Magari hayo yamekabidhiwa kwa Meneja wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Meneja wa Network Operations and Maintenance pamoja na Meneja wa Network Planning katika hafla iliyofanyika leo Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam. Makabidhiano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Aprili 29, 2026 ya kuendelea kuwekeza katika vitendea kazi ili kuongeza tija na ufanisi wa shirika.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mkurugenzi wa Ufundi wa shirika hilo, Mhandisi Cecil Francis, alisema ununuzi wa magari hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka 10 wa TTCL unaolenga kuboresha mazingira ya kazi, kuimarisha usimamizi wa miundombinu ya mawasiliano na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wateja.
Alisema magari hayo yataziwezesha timu za kiufundi kufika maeneo mbalimbali kwa wakati, kuimarisha usimamizi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kuhakikisha huduma za TTCL zinaendelea kutolewa kwa viwango vya juu.
"Magari haya ni mali ya Shirika. Ni wajibu wa watakaoyatumia kuyatunza, kuyatumia kwa kuzingatia maadili na kuhakikisha yanadumu ili yaendelee kutoa manufaa yaliyokusudiwa," alisema Mhandisi Francis.
Kwa upande wake, Meneja wa Network Operations and Maintenance (MNOM), Mhandisi Abbas Buge, aliyepokea magari hayo kwa niaba ya watumiaji, aliishukuru Menejimenti ya TTCL kwa kuendelea kuwekeza katika vitendea kazi vinavyowezesha utekelezaji bora wa majukumu ya kila siku.
Alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya Menejimenti ya TTCL ya kuboresha mazingira ya kazi na kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
"Kwa niaba ya wafanyakazi wote waliokabidhiwa magari haya, tunatoa shukrani za dhati kwa Menejimenti ya TTCL kwa kutuamini na kuendelea kuboresha vitendea kazi. Tunaahidi kuyatunza magari haya, kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha yanachangia kuongeza ufanisi wa kazi pamoja na kuboresha huduma kwa wateja wetu," alisema Mhandisi Buge.
Hatua hiyo inaendelea kudhihirisha dhamira ya TTCL ya kuwekeza katika rasilimali na miundombinu ya kazi ili kuongeza tija, kuimarisha utendaji wa shirika na kuhakikisha huduma bora za mawasiliano zinawafikia wananchi kwa haraka, ufanisi na ubora sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka 10 wa shirika.




