WAKULIMA WAFUNDISHWA MBINU RAHISI ZA KUHIFADHI CHAKULA, KUPUNGUZA UPOTEVU BAADA YA MAVUNO
Na Wellu Mtaki, Tanga
WAKULIMA nchini wamehimizwa kutumia mbinu bora za kuhifadhi mazao baada ya mavuno ili kupunguza upotevu wa chakula, kulinda ubora wa nafaka na kuhakikisha chakula kinapatikana kwa matumizi ya familia hadi msimu mwingine wa mavuno.
Wito huo unatolewa wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya chakula yanayofanyika mkoani Tanga, ambapo Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) unatoa elimu kuhusu teknolojia na mbinu mbalimbali za kuhifadhi nafaka, ikiwemo mahindi, mtama na mazao mengine ya chakula.
Akizungumza katika maadhimisho hayo,Afisa kilimo wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula ( NFRA ) Matay Hhando amesema elimu hiyo inalenga kuwasaidia wakulima kutunza chakula kwa usalama, hususan katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinazoweza kuathiri uzalishaji na upatikanaji wa chakula.
Amesema wakulima wanapaswa kuzingatia kanuni za uhifadhi bora, ikiwemo kuhakikisha nafaka zimekauka vya kutosha kabla ya kuhifadhiwa, ili kuzuia kuharibika kwa mazao na kupunguza hasara zinazoweza kujitokeza wakati wa kuyatunza.
Ameeleza kuwa katika uhifadhi wa nafaka kwenye maghala, magunia yanapaswa kupangwa vizuri juu ya vifaa vinavyoyainua kutoka sakafuni na kuwekwa kwa nafasi inayofaa kutoka ukutani, ili kuruhusu mzunguko wa hewa na kurahisisha ukaguzi wa hali ya mazao.
Aidha, amewashauri wakulima, hasa wanaohifadhi chakula katika ngazi ya kaya, kuepuka matumizi holela ya viuatilifu bila kuwa na uelewa na utaalamu unaohitajika, kutokana na uwezekano wa kuathiri afya za watu na kuongeza gharama za uzalishaji.
Badala yake, amesema wakulima wanaweza kutumia njia mbadala za kuhifadhi nafaka, zikiwemo mifuko maalumu ya kinga dhidi ya wadudu inayojulikana kama PICS, pamoja na vihenge vinavyofaa kwa uhifadhi wa nafaka, kwa kuzingatia maelekezo ya matumizi ya kila teknolojia.
Katika hatua nyingine, wakulima wamefundishwa njia rahisi za kutambua kama nafaka zimekauka vya kutosha kabla ya kuzihifadhi, ili kuepuka kuzihifadhi zikiwa na unyevu unaoweza kusababisha kuharibika.
Aidha ameeleza kuwa miongoni mwa njia za asili ni kusikiliza mlio wa nafaka zinapomiminwa kutoka chombo kimoja kwenda kingine, kuangalia sifa za punje na kutumia jaribio la chumvi na chupa.
Katika jaribio la chumvi na chupa, mkulima anatakiwa kuchukua sampuli ya nafaka na kuiweka ndani ya chupa ya plastiki iliyo safi na kavu, kisha kuongeza takribani vijiko viwili vya chakula vya chumvi na kutikisa mchanganyiko huo.
Baada ya hapo, chupa huwekwa kivulini kwa takribani dakika tano kabla ya kuangaliwa ili kuona kama chumvi imebadilika hali kutokana na unyevu uliopo kwenye nafaka.
Akizungumzia maendeleo ya teknolojia za uhifadhi, amesema wakala huo unaendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia teknolojia za kisasa, zikiwemo mifumo mikubwa ya kuhifadhi nafaka inayojulikana kama silo complexes.
Amesema wakala huo pia unaendelea na shughuli za uchakataji wa mazao na uzalishaji wa unga ulioongezewa virutubishi, hatua inayolenga kuchangia upatikanaji wa chakula chenye ubora wa lishe.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo unaendana na msisitizo wa ubunifu na lishe bora, huku akiwakaribisha wananchi na wadau kutembelea banda la wakala huo katika maadhimisho hayo ili kujifunza teknolojia zinazotumika kuhifadhi na kuongeza thamani ya mazao.
