Breaking News

TOSCI: MBEGU BORA NI MSINGI WA USALAMA WA CHAKULA NCHINI

 

Na. Wellu Mtaki,Tanga

MATUMIZI ya mbegu bora yanaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha kipato cha wakulima nchini, huku Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania

 (TOSCI) ikiimarisha elimu na huduma za kuwasaidia wakulima kupata mbegu zilizothibitishwa ubora.

Hata hivyo, pamoja na umuhimu huo, upatikanaji wa mbegu bora kwa wakati, gharama nafuu na karibu na maeneo wanayoishi wakulima ni miongoni mwa mambo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele ili kuwawezesha wakulima wengi zaidi kunufaika na kilimo chenye tija.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, mtafiti na mkaguzi wa mbegu wa TOSCI, Alex Kibaraza, amesema taasisi hiyo imeshiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kukutana moja kwa moja na wakulima na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu bora ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

Amesema usalama wa chakula hauwezi kutenganishwa na matumizi ya mbegu bora, kwa kuwa ni miongoni mwa nyenzo muhimu zinazomwezesha mkulima kuongeza uwezekano wa kupata mavuno yanayotarajiwa.

Kibaraza ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji unaofanyika katika tasnia ya mbegu, akieleza kuwa juhudi hizo zimechangia kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa mbegu nchini.

Amesema ili wakulima wengi wanufaike na mbegu bora, ni muhimu kuzingatia mambo matatu makuu ambayo ni upatikanaji wa mbegu za kutosha, urahisi wa kuzipata na uwezo wa wakulima kumudu gharama zake.

Ameeleza kuwa hatua ya kwanza ni kuhakikisha mbegu bora zinazalishwa kwa kiasi kinachokidhi mahitaji ya wakulima, huku hatua nyingine ikiwa ni kusogeza huduma za usambazaji karibu na wakulima, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wake, TOSCI inaendelea kusajili mawakala wa usambazaji wa mbegu ili kurahisisha upatikanaji wake na kupunguza usumbufu ambao wakulima wamekuwa wakikumbana nao wanapotafuta mbegu bora.

Amesema kadiri uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora unavyoimarika, ndivyo inavyoongezeka fursa ya kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuboresha upatikanaji wa pembejeo hizo muhimu katika shughuli za kilimo.

Katika hatua nyingine, Kibaraza amesema TOSCI imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu na huduma kwa wakulima ili kuwasaidia kupata taarifa sahihi kuhusu mbegu bora na namna ya kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza.

Amesema taasisi hiyo imeanzisha namba ya huduma kwa wateja 0800 782 424, inayowawezesha wakulima kuwasiliana na wataalamu kwa ajili ya kupata maelekezo kuhusu maeneo wanayoweza kununua mbegu bora au kutoa taarifa wanapokumbana na changamoto zinazohusiana na mbegu walizonunua.

Ameongeza kuwa kupitia huduma hiyo, mkulima anaweza kueleza eneo alilopo pamoja na aina ya mbegu anazohitaji ili kupata mwongozo kutoka kwa wataalamu wa taasisi hiyo.

Amesema huduma hiyo inalenga kuimarisha mawasiliano kati ya TOSCI na wakulima, ambao ni wadau muhimu katika kuhakikisha nchi inakuwa na uzalishaji wa kutosha wa chakula.

Kibaraza amesema mahitaji ya mbegu bora nchini yameendelea kuongezeka kutokana na kampeni za uhamasishaji zinazolenga kuwapa wakulima uelewa kuhusu faida za kutumia mbegu zilizothibitishwa ubora.

Amesema ongezeko hilo la mahitaji limechochea kampuni zinazozalisha mbegu kuongeza uzalishaji ili kuendana na mahitaji ya wakulima katika misimu mbalimbali ya kilimo.

Ameeleza kuwa matarajio ya TOSCI ni kuona uzalishaji wa mbegu bora nchini ukifikia tani 200,000 ifikapo mwaka 2030, huku lengo la uzalishaji kwa mwaka huu likiwa takribani tani 120,000.

Kwa mujibu wa Kibaraza, hadi wakati wa maelezo yake, uzalishaji ulikuwa tayari umevuka nusu ya lengo lililowekwa kwa mwaka husika.

Amesisitiza kuwa juhudi za kuhamasisha matumizi ya mbegu bora hazilengi zao moja pekee, bali zinahusisha mazao mbalimbali, pamoja na miche na vipando vinavyotumika katika shughuli za kilimo.

Mbali na kuimarisha usalama wa chakula, Kibaraza amesema uwekezaji katika uzalishaji wa mbegu nchini unaweza kuongeza fursa za biashara, kupanua ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Amesema TOSCI inaendelea kuweka mikakati ya kuvutia wawekezaji katika tasnia ya mbegu, ikiwemo kuwaelekeza maeneo na fursa zinazoweza kutumika kuanzisha au kupanua shughuli za uzalishaji.


Ameeleza kuwa kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini kunaweza pia kuiwezesha Tanzania kuuza mbegu katika masoko ya nje, hatua inayoweza kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, kampuni zinazozalisha mbegu, wasambazaji na wakulima ili kuhakikisha mbegu bora zinapatikana kwa urahisi na kutumika kwa wingi.

Amesema utekelezaji wa hatua hizo utasaidia kuongeza tija katika kilimo, kuboresha upatikanaji wa chakula na kuimarisha kipato cha wakulima pamoja na ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla.