Digital Tanzania yabadili huduma za Serikali kwa teknolojia
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Priscus Kiwango, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya kidijitali na utoaji wa huduma za umma kwa njia ya kielektroniki kupitia Mradi wa Digital Tanzania (DTP).
Kiwango amesema mradi huo ulioanza mwaka 2021 kwa ufadhili wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 150 kutoka Benki ya Dunia, umewezesha kuboresha miundombinu ya mawasiliano, kuongeza upatikanaji wa intaneti na kurahisisha utoaji wa huduma za Serikali kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni kujengwa na kuboreshwa kwa miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo minara katika maeneo ya vijijini yaliyokuwa hayana huduma ya uhakika, ambapo wananchi sasa wanaweza kupata mawasiliano kupitia mitandao ya 3G na 4G, huku taasisi za Serikali hadi ngazi ya Serikali za Mitaa zikiunganishwa katika mifumo ya kidijitali.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Mradi wa Digital Tanzania, Bakari Mwamguguyo, mradi huo unatekelezwa katika maeneo makuu matatu ambayo ni Ekolojia ya Kidijitali inayohusisha sheria, miongozo na sera za TEHAMA, Uunganishaji wa Kidijitali pamoja na ujenzi wa uwezo wa watumishi. Amesema kupitia mradi huo, minara mipya 758 imejengwa na mingine 304 imeboreshwa kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G.
Aidha, Serikali imeongeza uwezo wa intaneti kwa Gbps 60, ambapo Gbps 40 ni kwa Tanzania Bara na Gbps 20 kwa Zanzibar, hatua inayosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti na kupunguza gharama za matumizi kwa taasisi za umma.
Mradi huo pia umewezesha kuanzishwa kwa vituo 32 vya huduma pamoja (One-Stop Service Centers) katika majengo ya Posta, vinavyowawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali, ikiwemo NIDA, RITA, Jeshi la Polisi na Land Registry katika eneo moja.
Katika kujenga uwezo wa watumishi, amesema watumishi wa umma 500 wamepatiwa mafunzo kuhusu teknolojia za kisasa, ikiwemo matumizi ya akili bandia (Artificial Intelligence), huku watumishi 50 wakipelekwa kusoma nje ya nchi katika ngazi ya Uzamili katika mataifa mbalimbali yakiwemo India, Singapore, China, Estonia, Finland na Malaysia. Mradi huo pia umewezesha mifumo kama PEPMIS na Mfumo wa Daktari wa Huduma za Serikali ambao unasaidia wananchi kupata taarifa kuhusu huduma, muda wa kuzipata na gharama zake.
Mradi wa Digital Tanzania unatarajiwa kukamilika rasmi Oktoba 31, 2026, huku Serikali ikiwa imeanza mazungumzo na Wizara ya Fedha pamoja na Benki ya Dunia kuhusu uwezekano wa kuingia katika awamu ya pili.
Awamu hiyo inalenga kuendeleza na kukamilisha maeneo ambayo hayajakamilishwa katika awamu ya kwanza, pamoja na kuimarisha zaidi matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

