Breaking News

BUILD EXPO TANZANIA 2026 YAWAKUTANISHA WADAU WA UJENZI DAR

 

Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam 

Maonesho ya 27 ya Kimataifa ya Ujenzi na Ujenzi wa Majengo (Buildexpo Tanzania 2026) yanatarajiwa kufanyika Septemba 23 hadi 25, mwaka huu, katika Kituo cha Maonesho cha Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, yakilenga kuwakutanisha wadau wa sekta ya ujenzi, teknolojia ya maji, utengenezaji wa bidhaa za mbao na taa.

Maonesho hayo yatazinduliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard D. Akwilapo, huku yakihudhuriwa na mabalozi, viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi.

Kwa mujibu wa waandaaji, maonesho hayo yataenda sambamba na Afriwood, Watertech na Lightexpo Tanzania 2026, yakitoa fursa kwa washiriki kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mahusiano ya kibiashara kupitia maonesho ya bidhaa na teknolojia mbalimbali.

Maonesho hayo yanatarajiwa kushirikisha waonyeshaji kutoka zaidi ya nchi 30, zikiwemo China, Uturuki, Ujerumani, Ureno, India, Tanzania na Kenya. Washiriki watapata fursa ya kuona bidhaa na teknolojia za kisasa zinazolenga kuendeleza sekta ya ujenzi na miundombinu katika Tanzania na nchi jirani.

Buildexpo Tanzania inaungwa mkono na taasisi mbalimbali, ikiwemo Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Chama cha Wasanifu Majengo Tanzania (AAT), Taasisi ya Wahandisi Tanzania, TUCASA na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA). 

Waandaaji wametoa wito kwa wasanifu majengo, wahandisi, wakandarasi, wawekezaji na wadau wengine kuhudhuria maonesho hayo, ambapo kiingilio kwa wageni wa kibiashara ni bure.