VETA- Kihonda Yabuni Teknolojia ya Kuhifadhi Mazao, Kuongeza Kipato kwa Wakulima
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Utumiaji wa teknolojia ya cold room umeelezwa kuwa suluhisho la kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza kipato kwa wakulima na wafanyabiashara, kufuatia ubunifu uliofanywa na Chuo cha Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) Kihonda.
Ubunifu huo umebuniwa na mwalimu wa fani ya Refrigeration and Air Conditioning, Masumbuko Malko Maliganya, ambaye alisema mfumo huo unamwezesha mkulima kuhifadhi mbogamboga, matunda na mazao mengine kwa zaidi ya wiki tatu badala ya kuyauza kwa bei ya hasara wakati wa mavuno mengi.
Alisema teknolojia hiyo inampa mkulima nafasi ya kusubiri kipindi ambacho bei za mazao zitakuwa nzuri, hivyo kupunguza hasara zinazotokana na kuharibika kwa bidhaa au kushuka kwa bei sokoni.
Maliganya alibainisha kuwa mfumo huo unaweza pia kutumiwa na wafanyabiashara wadogo, hususan wauzaji wa mbogamboga, matunda, maziwa na bidhaa nyingine zinazohitaji kuhifadhiwa kwenye ubaridi ili zidumu kwa muda mrefu.
Aidha, alisema cold room hiyo imegawanywa katika sehemu maalumu zinazowezesha kuhifadhi bidhaa mbalimbali ikiwemo nyama, samaki, maziwa, vinywaji na mazao ya shambani, jambo linalorahisisha matumizi kwa biashara tofauti.
Alisisitiza kuwa ubunifu huo unaonyesha mchango wa VETA katika kutoa suluhisho la changamoto za wananchi kupitia teknolojia, huku ukichochea ongezeko la thamani ya mazao, kupunguza upotevu wa chakula na kuimarisha sekta za kilimo na mifugo nchini.
