Mkurugenzi COASCO: Ushirika Waimarisha Kilimo na Uchumi
Na Hawa Ismail-Dar es Salaam
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Jeremiah Mugeta, amesema sekta ya ushirika inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza kilimo na uchumi wa Taifa kupitia usimamizi madhubuti na ukaguzi unaoongeza uwazi na uwajibikaji.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la Wizara ya Kilimo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Mugeta alisema taasisi zilizo chini ya wizara hiyo zimeonesha mafanikio makubwa kwa kutoa elimu, bidhaa na huduma zinazochochea maendeleo ya sekta ya kilimo na ushirika.
Alisema takwimu zinaonesha sekta ya kilimo inachangia zaidi ya asilimia 26 ya Pato la Taifa, huku mazao yanayozalishwa kupitia vyama vya ushirika yakichangia zaidi ya dola bilioni mbili za Marekani kwa mwaka, jambo linalodhihirisha mchango mkubwa wa ushirika katika uchumi wa nchi.
Mugeta alisema COASCO imejipanga kuhakikisha vyama vya ushirika vinaendelea kuwa imara kwa kufanya ukaguzi wa kitaalamu, kutoa elimu kwa wanachama na viongozi, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa sheria na kanuni za uendeshaji wa vyama hivyo.
Alibainisha kuwa kuanzia Julai 20, 2026, shirika hilo litaanza awamu ya kwanza ya ukaguzi wa vyama vya ushirika kwa mwaka wa fedha 2026/27, huku akiwataka viongozi wa vyama kuwasilisha taarifa za fedha kwa wakati ili kurahisisha zoezi hilo.
Aidha, alisema hali ya usimamizi wa vyama vya ushirika imeendelea kuimarika, ambapo asilimia 16 ya vyama sasa vinapata hati safi za ukaguzi, ikilinganishwa na asilimia nne ya miaka iliyopita, hatua inayodhihirisha ongezeko la uwazi na uwajibikaji katika sekta hiyo.
Mugeta aliipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Kilimo kwa kuendelea kuimarisha taasisi za ushirika, akisisitiza kuwa COASCO itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu ili kuongeza imani ya wanachama, kuimarisha ushirika na kuchochea maendeleo ya kilimo nchini.
