Nyansaho Aisifu JKT kwa Kuongeza Fursa za Ajira
Na Hawa Ismail, Dar es Salaam
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linaendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza ajira na kuwawezesha vijana kujitegemea kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam, Dkt. Nyansaho alisema mafanikio ya JKT yanaonekana kupitia miradi ya uzalishaji pamoja na mafunzo yanayotolewa kwa vijana ili kuwajengea ujuzi wa kujiajiri.
Alitaja kampuni ya usafi na unyunyuzi dawa ya SUMAJKT kuwa ni miongoni mwa miradi yenye mafanikio, akisema imefanikiwa kutoa ajira kwa vijana 4,800, hatua inayochangia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Aidha, aliwapongeza viongozi wa JKT na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuendelea kusimamia ulinzi na usalama wa nchi, akisisitiza kuwa hali ya amani ndiyo msingi wa maendeleo na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Nyansaho alisema maonesho ya Sabasaba yameziwezesha taasisi hizo kuonesha huduma mbalimbali wanazotoa kwa wananchi, pamoja na nafasi ya kueleza mchango wao katika maendeleo ya taifa kupitia mafunzo, uzalishaji mali na ulinzi wa nchi.
