Dkt. Munisi: Serikali Yaongeza Kasi Kukuza Ujuzi wa Nguvu Kazi
Na Hawa Ismail-Dar es Salaam
Serikali imesema inaendelea kuimarisha programu za ukuzaji wa ujuzi kwa nguvu kazi na kuboresha upatikanaji wa huduma za umma katika jitihada za kuimarisha ajira, mahusiano kazini na mifumo ya hifadhi ya jamii nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Dkt. Evaline Wilbard Munisi, baada ya kutembelea mabanda ya taasisi za Serikali katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Dkt. Munisi alisema taasisi zilizo chini ya wizara yake zinatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria za kazi, afya na usalama mahali pa kazi, viwango vya chini vya mishahara na haki za wafanyakazi, sambamba na kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wanaotembelea mabanda hayo.
Aliwapongeza watumishi wanaotoa huduma kwenye maonesho hayo kwa weledi na ubunifu wao, akisema wamechangia kuongeza uelewa wa wananchi na kupunguza sintofahamu kuhusu masuala ya kazi kupitia utoaji wa elimu ana kwa ana.
Dkt. Munisi alisema Serikali imeongeza msisitizo katika programu za kukuza ujuzi kwa vijana ili kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira linalobadilika kwa kasi.
Alisema programu hizo tayari zinaendelea kutekelezwa, huku akibainisha kuwa hivi karibuni alitembelea baadhi ya vyuo vya mafunzo ya ufundi na stadi ili kukagua maendeleo ya utekelezaji wake.
"Baada ya miaka michache tunaamini Tanzania haitahitaji tena kutegemea wataalamu kutoka nje katika maeneo mengi kwa sababu tunawaandaa wataalamu wetu hapa nchini," alisema Dkt. Munisi, akieleza kuwa mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga taifa lenye rasilimali watu wenye ujuzi na ushindani.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kudumisha mahusiano mazuri kazini na katika jamii kwa ujumla, akisema Serikali inaendelea kushirikiana na taasisi za dini, vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine ili kuimarisha umoja wa kitaifa na mshikamano wa kijamii.
"Mahusiano mazuri ndiyo lango la maendeleo," alisema, huku akiwahimiza Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na ushirikiano.
Katika ziara hiyo, Dkt. Munisi pia alitembelea mabanda ya Taasisi ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ambako alijionea utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.
Alizipongeza taasisi hizo kwa utoaji wa huduma kwa ufanisi na kusema matumizi ya mifumo ya kidijitali, hususan NSSF, yamerahisisha wanachama kupata taarifa za michango, mafao na huduma nyingine kwa wakati halisi.
Dkt. Munisi aliwahimiza wananchi kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na mabanda mengine ya Serikali katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata huduma na taarifa mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.
Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam ni miongoni mwa maonesho makubwa zaidi ya biashara Afrika Mashariki, yakileta pamoja taasisi za Serikali, sekta binafsi na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi kuonesha bidhaa, huduma na fursa za uwekezaji.
