GASCO Yaongeza Ufanisi wa Miundombinu ya Gesi
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
KAMPUNI ya GASCO imesema inaendelea kuimarisha miundombinu ya gesi asilia nchini ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia watumiaji kwa uhakika na kuchangia maendeleo ya sekta ya nishati na uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mhandisi Mitambo wa GASCO, Daud Enock, amesema kampuni hiyo inayomilikiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ina jukumu la kuendesha, kusimamia na kufanya matengenezo ya miundombinu yote ya gesi asilia inayomilikiwa na shirika hilo.
Amesema GASCO inasimamia mitambo miwili ya kuchakata gesi asilia, ambayo ni wa Songosongo wenye uwezo wa kuchakata futi za ujazo milioni 140 kwa siku na wa Mtwara wenye uwezo wa kuchakata futi za ujazo milioni 210 kwa siku.
Enock amesema baada ya gesi kuchakatwa, husafirishwa kupitia bomba la gesi hadi Kinyerezi, Dar es Salaam, ambako husambazwa kwa matumizi ya kuzalisha umeme, viwandani, taasisi mbalimbali na majumbani.
Aidha, amesema kampuni hiyo pia inaendelea kujenga miundombinu mipya ya kusambaza gesi pale miradi mipya inapopatikana, ili kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma hiyo nchini.
Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha uliopita, GASCO ilitekeleza miradi sita ya ujenzi wa miundombinu ya gesi katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, ikiwemo kuunganisha huduma kwa wateja wapya wa viwandani na kibiashara.
Kuhusu changamoto, Enock amesema kampuni inakabiliwa na baadhi ya taratibu za manunuzi, lakini hazijazuia utekelezaji wa majukumu yake, akisisitiza kuwa GASCO itaendelea kuboresha miundombinu ya gesi ili kuhakikisha huduma inakuwa salama, ya kuaminika na endelevu.
