RAIS SAMIA KUFUNGUA TMIC 2026, WASHIRIKI ZAIDI YA 2,000 KUTOKA MATAIFA 50 KUKUTANA DAR ES SALAAM KUJADILI UWEKEZAJI NA UONGEZAJI THAMANI YA MADINI.
Na Mwandishi wetu., Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua rasmi Mkutano wa Saba wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026) utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam. Mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 2,000, watoa mada zaidi ya 100 na wadau wa sekta ya madini kutoka mataifa zaidi ya 50 duniani.
Akizindua rasmi maandalizi ya mkutano huo leo Juni 27, 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kaulimbiu ya TMIC 2026 ni “Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi,” ikiwa inalenga kuhamasisha uwekezaji katika uchakataji na uyeyushaji wa madini ili kuongeza thamani ya rasilimali za nchi na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji wa madini barani Afrika.
Mavunde amesema Serikali imejipanga kujenga uchumi wa viwanda unaotokana na madini kwa kuwekeza katika miradi ya uongezaji thamani badala ya kuuza malighafi. Amesema Tanzania tayari ina viwanda vinane vya kusafisha dhahabu, huku viwanda vingine vikiendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Dodoma, pamoja na miradi mikubwa ya uchakataji wa nikeli, shaba, Heavy Mineral Sands na niobium.
Ameongeza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 600 zinawekezwa katika ujenzi wa kiwanda cha chuma kitakachotumia malighafi za ndani kwa asilimia 100. Aidha, thamani ya manunuzi kupitia mpango wa Local Content imefikia shilingi trilioni 5.1, hatua inayoonesha kuongezeka kwa ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, sekta ya madini imeingiza shilingi trilioni 1.374 katika Mfuko Mkuu wa Serikali, kiwango kilichovuka lengo la shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka huu wa fedha. Serikali pia imeidhinisha asilimia 10 ya mapato ya sekta hiyo kuelekezwa katika utafiti wa kina wa jiofizikia ili kuongeza maeneo yanayofahamika kuwa na madini kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, sambamba na kuanzisha mfuko maalumu wa mikopo kwa wachimbaji wadogo.
Naye Katibu Mtendaji wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, amesema TMIC 2026 itajadili zaidi ya mada 20 zinazohusu sera, kodi, uwekezaji, teknolojia, nishati safi, madini ya kimkakati, uongezaji thamani na masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG). Amesema mkutano huo pia utaweka mkazo katika maendeleo ya wachimbaji wadogo pamoja na ushirikishwaji wa wanawake na watu wenye ulemavu, huku ukitarajiwa kufungwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)