DIWANI MBOGA AAHIDI KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WA DINI
Na Mwandishi Wetu
Diwani wa Kata ya Makangarawe, Fadhili Mboga, amesema kuna umuhimu kwa taasisi za dini kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ili ziweze kujitegemea na kutekeleza majukumu yake ya kiroho na kijamii kwa ufanisi zaidi.
Amesema ushirikiano kati ya viongozi wa dini na Serikali utasaidia makanisa na taasisi nyingine za dini kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo zinazotolewa na halmashauri.
Mboga alitoa kauli hiyo Juni 27, 2026, aliposhiriki Ibada Maalumu ya Sabato ya Mashemasi iliyofanyika katika Kanisa la Waadventista Wasabato Dovya. Aliwapongeza waumini wa kanisa hilo kwa mshikamano, upendo na mchango wao katika maendeleo ya Kata ya Makangarawe.
Aliahidi kushirikiana na uongozi wa kanisa ili kuhakikisha linapata fursa za mikopo kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, hatua ambayo alisema italiwezesha kuanzisha na kuendeleza miradi ya kiuchumi itakayoongeza uwezo wake wa kujitegemea.
"Naahidi baada ya tukio hili tuwasiliane ili kanisa liweze kujitegemea katika shughuli za kiuchumi.
"Nitahakikisha tunawawezesha kupata mikopo kupitia halmashauri," alisema Mboga.
Aidha, Mboga alisisitiza nafasi muhimu ya viongozi wa dini katika kujenga taifa lenye maadili, umoja na amani. Aliwataka kuendelea kuhubiri amani na mshikamano ili Tanzania iendelee kuwa salama na yenye utulivu.
Katika kuunga mkono shughuli za maendeleo ya kanisa hilo, Mboga alisema tayari amechangia jumla ya shilingi 750,000 kwa ajili ya kusaidia mahitaji mbalimbali ya kanisa.
Kwa upande wake, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Temeke, Jacob Chenga, alisema Mbunge wa Jimbo hilo, Mariam Kisangi, amechangia shilingi 500,000 na kuahidi kuwa waumini wa kanisa hilo wataendelea kushirikishwa fursa za kiuchumi zinazotolewa kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
Chenga alisema ushirikishwaji huo utasaidia kanisa kuanzisha miradi endelevu ya maendeleo itakayoliwezesha kujitegemea, ikiwemo uchimbaji wa kisima, ununuzi wa mabenchi, gari la huduma za kiroho, mahema pamoja na kuboresha miundombinu na vifaa muhimu vinavyohitajika kanisani.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Kata wa Makangarawe wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) Julius Mkada naye alichangia kiasi cha shilingi 150000 kama kuunga mkongo na kuonesha umuhimu wa viongozi wa dini katika jamii.





