Breaking News

RAIS MSTAAFU DKT KIKWETE AMPONGEZA MTANZANIA NGASUMA EVA KANYEKA ALIYENG'ARA CHUO KIKUU CHA HAVARD NCHINI MAREKANI KWA KUSHINDA TUZO YA TESSA JOWELL FOUNDATION

 


Na Mwandishi Wetu 

Akiwa katika Chuo Kikuu cha Harvard, jijini Cambridge, jimbo la Massachusetts, nchini Marekani, Rais Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amempongeza mwanafunzi wa Kitanzania wa Shahada ya Uzamivu (PhD), Bi. Ngasuma Eva Kanyeka, kwa kushinda tuzo inayotolewa na Programu ya Uongozi wa Mawaziri ya Chuo Kikuu cha Harvard (Harvard Ministerial Leadership Program – HMLP), inayodhaminiwa na taasisi ya Tessa Jowell Foundation.

Tuzo hiyo yenye ushindani mkubwa hutolewa kila mwaka kwa mwanafunzi mmoja wa PhD wa Harvard anayefanya utafiti unaochangia maendeleo ya nchi zinazoendelea. Tuzo hiyo inatolewa kwa udhamini wa Tessa Jowell Foundation, taasisi iliyoanzishwa kuenzi mchango wa marehemu Baroness Tessa Jowell, aliyekuwa kinara wa kuhimiza mifumo ya afya yenye huruma na maendeleo jumuishi ya utotoni.

Kwa sasa, taasisi hiyo inaongoza juhudi za kimkakati katika kuboresha matibabu na huduma za saratani ya ubongo, pamoja na kuimarisha maendeleo ya awali ya mtoto. Kupitia uchangishaji fedha, ushawishi wa sera na ushirikiano mpana, inaunganisha wadau kutoka NHS, serikali, vyuo vikuu na asasi za kiraia ili kuleta mageuzi endelevu katika sekta ya afya na ustawi wa watoto.

Utafiti wa Bi. Kanyeka unatumia teknolojia ya akili mnemba (Artificial Intelligence) kuboresha mifumo ya dhamana ya mikopo (AI credit models), kwa lengo la kuwawezesha wanawake na vijana kupata mikopo nafuu, kuongeza kipato na kuboresha afya ya kaya.

Bi. Kanyeka ni miongoni mwa wanafunzi wachache wa Kitanzania waliopata nafasi ya kusomea Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Harvard tangu kuanzishwa kwake mwaka 1636, na ndiye wa kwanza kushinda tuzo hiyo ya kifahari.

Rais Mstaafu Dkt. Kikwete alimpongeza kwa kuiwakilisha vyema Tanzania katika jukwaa la kimataifa na kuitangaza nchi kwa heshima kubwa ndani ya Chuo Kikuu cha Harvard.