Breaking News

Ulega awataka TBA kuhakikisha wanapangishwa vijana kwa kuzingatia vigezo kwenye mradi wa Nyumba za Temeke Kota

 



 

Na Mwandishi Wetu- Dar es salaam

 Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameuagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha upatikanaji wa nyumba katika mradi wa Temeke Kota unazingatia vigezo bila vikwazo, akisisitiza kuondoa vitendo vya udalali na upendeleo kwa watumishi wapya na wananchi kwa ujumla.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Mei 3,2026 wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo, Ulega amesema mradi huo una jumla ya nyumba 144, zikiwemo 72 za chumba kimoja na 72 zenye vyumba vya kulala (master). 

Ulega amesema lengo ni kuwasaidia wananchi, hususan vijana wanaoanza maisha na ajira, kupata makazi ya gharama nafuu.

“Hii ni kazi ambayo ameielekeza Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunatafuta suluhu ya nyumba za bei nafuu kwa wananchi, hasa vijana wanaoingia kwenye utumishi wa umma na wale wanaoanza maisha,” amesema Ulega.

Aidha, ameitaka TBA kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kuongeza kasi ya maendeleo, akieleza kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya maelekezo ya Rais katika kuharakisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Uzairu Athumani, ameushukuru serikali kwa kupeleka mradi huo katika eneo hilo na kueleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake.

“Sisi Wanatemeke tunakuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalam wa ujenzi. Pia tumepokea maelekezo ya Waziri kuhakikisha mchakato wa upangishaji unakuwa wazi ili walengwa wa kipato cha chini wanufaike,” amesema Athumani.