Breaking News

TAMISEMI Yarahisisha Huduma Sabasaba

 

Na Hawa Ismail, Dar es Salaam

Wananchi wanaotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) wameendelea kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa sehemu moja, hatua inayorahisisha upatikanaji wa taarifa na utatuzi wa changamoto bila kutembelea ofisi tofauti.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo Julai 10, 2026, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif, alisema mfumo huo umeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa kuwa unawakutanisha wananchi na wataalamu kutoka idara na taasisi zote za TAMISEMI.

Alisema wananchi wanapata ushauri na ufafanuzi kuhusu huduma mbalimbali zikiwemo elimu, ujenzi, uhamisho wa watumishi, vibali pamoja na masuala mengine yanayosimamiwa na mamlaka za serikali za mitaa.

Aidha, alieleza kuwa banda hilo pia linatoa huduma kutoka taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu zinazoshughulikia hifadhi ya jamii, watu wenye ulemavu, udhibiti wa dawa za kulevya na huduma nyingine za kijamii.

Dkt. Seif aliwataka wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kutumia fursa hiyo kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na TAMISEMI pamoja na kufikisha changamoto zao ili zipatiwe ufumbuzi kwa haraka.