DC Msando Aitaka Ubungo Kuimarisha Ushirikiano na Wananchi Kutatua Changamoto za Miundombinu ya Shule
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amezitaka Halmashauri pamoja na Kamati za Maendeleo za Kata kushirikiana kwa karibu na wananchi katika kutatua changamoto za miundombinu ya shule, hususan uhaba wa madarasa, ofisi za walimu na vyoo.
Akizungumza katika Baraza la Ushauri la Wilaya la Jiji la Dar es Salaam lililofanyika Februari 09, 2026, Msando amesema bado kuna shule kadhaa ndani ya Wilaya ya Ubungo ambako walimu wanalazimika kutumia korido kama ofisi au kubanana katika chumba kimoja kutokana na uhaba wa maeneo ya kufanyia kazi, hali inayopunguza ufanisi wao katika utekelezaji wa majukumu.
Amesisitiza kuwa pamoja na serikali kuwa na vipaumbele vingi vya maendeleo, suala la kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu linapaswa kupewa uzito wa kipekee, kwa kuwa lina mchango mkubwa katika kuboresha utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi.
Katika hatua nyingine, Msando ameeleza kuwa uongezaji wa matundu ya vyoo shuleni unahitaji juhudi za pamoja, akibainisha kuwa baadhi ya kamati za shule na kamati za maendeleo za kata zimekuwa zikitegemea zaidi Halmashauri badala ya kuwashirikisha wananchi kikamilifu katika kutatua changamoto hizo.
“Serikali inaendelea kukusanya na kutoa fedha kwa ajili ya maboresho mbalimbali, lakini kamati za shule na kamati za maendeleo za kata zina wajibu wa kuwahamasisha wananchi kushiriki. Hata michango ya wafadhili inaweza kusaidia kuongeza matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari,” amesema Msando.
Ameongeza kuwa licha ya serikali kutoa elimu bila malipo, kuajiri walimu na kujenga miundombinu, hali hiyo haipaswi kuwafanya wananchi kulegeza juhudi zao katika kuchangia maendeleo ya jamii.
Vilevile, Msando ameielekeza Halmashauri ya Ubungo kufanya tathmini ya masoko yenye uwezo wa kutoa ajira na huduma kwa wananchi, ili yafanyiwe maboresho na kuchangia kukuza uchumi wa wilaya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo, Aron Kagurumjuli, amesema kuwa kipaumbele cha Halmashauri ni uchongaji wa madawati na ujenzi wa madarasa mapya ili kupunguza upungufu wa miundombinu uliopo katika shule za wilaya hiyo.

