DC Temeke Awataka Madiwani Kuhakikisha wanasimamia maendeleo Temeke
Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amewataka madiwani wa Manispaa ya Temeke kutekeleza kikamilifu maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha barabara zinazoelekea katika maeneo ya kiuchumi, ikiwemo masoko, zinakuwa katika hali nzuri ili kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa ufanisi.
Akizungumza leo Februari 10, 2026, katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo, Mapunda amesema ni muhimu kwa madiwani kukaa kwa pamoja, kutambua changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi, hususan katika sekta ya elimu, ikiwemo uhaba wa madarasa, kwa kutumia mapato ya ndani ya Manispaa ya Temeke.
Mapunda ameongeza kuwa madiwani wanapaswa kuangalia upya habibu za rejea za miradi ya awamu zilizopita ambayo haikutekelezwa au haikukamilika, ili kuhakikisha inaendelea na kukamilishwa kwa wakati kwa manufaa ya wananchi.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuchagua maeneo korofi ndani ya manispaa hiyo na kuyatafutia suluhisho la kudumu, ili kuboresha huduma na maisha ya wananchi.
“Uongozi ni amana. Wananchi wametupa dhamana ya kuwatumikia na kuwaletea matokeo chanya,” amesisitiza Mapunda.
Aidha, Mapunda amewataka madiwani kuwa daraja kati ya changamoto za wananchi na wawekezaji, kwa kuhakikisha mazingira bora ya uwekezaji yanakuwepo ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Manispaa ya Temeke.



