Tamasha la Sauti za Busara 2026 Lathibitisha Ratiba Kamili huku Tiketi za Mwisho Zikiuzwa kwa Kasi Kabla ya Tamasha la Februari, Stone Town – Zanzibar
Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
Zanzibar- Tanzania
Zikiwa zimesalia wiki mbili tu kabla ya ufunguzi wa toleo la 23 la tamasha la Sauti za Busara, hamasa na matarajio yanaendelea kuongezeka Zanzibar na kwingineko. Maandalizi ya mwisho yanaendelea kwa kasi kuelekea tamasha linalojulikana kama “Tamasha Rafiki Zaidi Duniani”, litakalofanyika kuanzia Alhamisi tarehe 5 hadi Jumapili tarehe 8 Februari 2026, likitanguliwa na ufunguzi wa awali (soft opening) siku ya Jumatano tarehe 4 Februari, katika makao yake mapya — Uwanja wa Mnazi Mmoja, Stone Town.
Kufuatia tangazo la hivi karibuni la kuhamia katika eneo jipya lenye ukubwa zaidi, Busara Promotions imethibitisha kuwa uamuzi huo umeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kupokea hadhira kubwa, kuboresha mtiririko wa wageni, pamoja na kuinua uzoefu wa wasanii na watazamaji. Kwa zaidi ya miaka 22, Ngome Kongwe imekuwa kitovu cha kihistoria cha tamasha, ikitoa mazingira ya karibu na ya kipekee.
Hata hivyo, mwaka 2026 unaashiria hatua mpya ya mageuzi kwa kuhamia Mnazi Mmoja — eneo lenye nafasi pana, mandhari ya kijani, hewa ya bahari, pamoja na faida za kiusalama, upatikanaji rahisi na fursa za ukuaji wa baadaye. Kiuchumi, eneo hili linaruhusu wauzaji wengi zaidi, hadhira kubwa na programu zilizopanuliwa kiutamaduni, linaendeleza maadili ya tamasha bila kusimama palepale.
Zaidi ya majukwaa makuu, programu za pembeni (fringe programmes) za Sauti za Busara zinaendelea kuongeza athari zake. Msafara wa Carnival Parade hubadilisha Stone Town kuwa jukwaa linalotembea, ukifuta mipaka kati ya msanii na mtazamaji. Swahili Encounters huwakutanisha wanamuziki kutoka nchi mbalimbali kwa mazoezi na maonesho ya pamoja, zikisisitiza mchakato wa ubunifu kuliko maonesho pekee.
Aidha, majukwaa ya kitaaluma kama Movers & Shakers hutoa nafasi muhimu kwa mijadala ya kitaalamu — nguzo muhimu ya uchumi endelevu wa ubunifu ambayo mara nyingi hupuuzwa.
Tamasha pia linafika nje ya Stone Town kupitia Busara Plus, jukwaa la bure la jamii litakalofanyika Fumba Town, Nyamanzi.
Upanuzi huu wa kijiografia unaimarisha dhana kwamba utamaduni unapaswa kusambaa, si kujikita eneo moja. Kwa vijana na wasanii chipukizi, jukwaa hili linatoa fursa ya kujitokeza bila vikwazo vya kifedha — hatua ndogo kiuchumi, lakini yenye thamani kubwa kiutamaduni.
Ujumuishi wa Kijinsia na Miundombinu Bora
Ujumuishi wa kijinsia unaendelea kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa tamasha. Wanawake wanaonekana si tu kama wasanii, bali pia kama waandaaji, wasimamizi, watayarishaji na mafundi wa kiufundi. Katika sekta ambayo mchango wa wanawake mara nyingi hautambuliwi ipasavyo, Sauti za Busara inaweka mfano wa kimyakimya lakini thabiti — ambapo uwakilishi unakuwa sera, na usawa unakuwa vitendo.
Uwanja wa Mnazi Mmoja utakuwa na majukwaa kadhaa, maeneo ya wazi yenye kivuli chini ya miti ya karne nyingi, soko lililopanuliwa la chakula na kazi za mikono, maeneo ya mitandao ya kitaaluma, pamoja na miundombinu iliyoboreshwa kwa watembea kwa miguu, usafiri wa umma na magari.
Mahitaji Makubwa ya Tiketi na Wasanii Wakubwa
Mahitaji ya tamasha la 2026 yamevunja rekodi. Tiketi za Early Bird zimekwisha kabisa, huku Advance Tickets zikiendelea kuuzwa kwa kasi. Hali hii inachochewa na ratiba ya kimataifa inayoshirikisha zaidi ya wanamuziki 400 kutoka nchi 21 barani Afrika na duniani kote.
Kinara wa tamasha ni gwiji wa muziki kutoka Mali, Salif Keita, ambaye urithi wake wa muda mrefu na wimbo wake uliovuma kimataifa “Yamore” umevutia mashabiki wa zamani na kizazi kipya duniani kote.
“Mwitikio wa mwaka huu umekuwa wa kipekee sana,” alisema Journey Ramadhan, Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara.
“Mchanganyiko wa eneo jipya lenye uwezo mkubwa, orodha bora ya wasanii inayoongozwa na Salif Keita, pamoja na ongezeko la hamasa ya kimataifa, umeifanya Sauti za Busara 2026 kuwa moja ya matoleo yanayosubiriwa kwa hamu zaidi katika historia yetu. Ushirikiano wetu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mamlaka husika umetuwezesha kupanua tamasha kwa usalama na ubora.”
Athari za Kijamii na Programu Maalum
Zaidi ya muziki, Sauti za Busara 2026 inaendelea kujitofautisha kupitia mchango wake wa kijamii na kitamaduni. Utekelezaji wa kwanza wa mpango wa “Inspire to Lead!” ulifanyika kwa mafanikio tarehe 17 Januari 2026 katika Uwanja wa Kibanda Maiti, ukivutia ushiriki mkubwa na mrejesho chanya.
Programu hii itaendelea wakati wote wa tamasha kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Umoja wa Ulaya, na UN Women, ikiwa sehemu ya Gender Transformative Action Programme unaolenga kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, kukuza uongozi wa wanawake, na kuendeleza kampeni kama Tokomeza Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na Rijali Anajali.
“Jukwaa letu linatuwezesha kuwafikia maelfu ya watu kupitia utamaduni,” alisema Zakialulu Mdemu, Afisa Programu wa Busara Promotions.
“Kwa kuunganisha programu hizi ndani ya tamasha, tunaongeza uelewa kuhusu Vituo vya Huduma za Kijinsia (One-Stop Gender Centres) na huduma muhimu zinazotolewa na Serikali ya Zanzibar, huku tukisherehekea uongozi, uthabiti na usawa.”
Wakati huohuo, Busara Promotions imeripoti mwitikio mkubwa kwa mpango wa Gender@Work Tanzania, uliopokea maombi 179 kutoka nchi 11. Mpango huu unalenga kuwajengea wanawake uwezo katika nafasi za kitaaluma na kiufundi ndani ya sekta ya muziki wa moja kwa moja na matukio, ikiwemo usimamizi wa majukwaa, uzalishaji na uratibu wa wasanii. Mpango huu unatekelezwa kwa ushirikiano na Music In Africa Foundation na umechangia kuwainua mamia ya wanawake katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kupitia mradi wa Amplifying Women’s Voices.
Zanzibar ikijiandaa kwa mojawapo ya misimu yake yenye shughuli nyingi zaidi za kitamaduni, Sauti za Busara 2026 inaahidi siku nne za muziki wa nguvu, kubadilishana tamaduni, athari za kijamii na sherehe kubwa katika Uwanja wa Mnazi Mmoja, Stone Town. Kutokana na ongezeko la mahitaji ya tiketi na idadi ya wageni wa kimataifa, waandaaji wanawahimiza wadau kununua tiketi mapema na kupanga safari zao kwa wakati.
