Mwakibinga Ampongeza Rais Samia kwa Kusimamia Uhuru wa Mahakama na Maendeleo ya Kisheria
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Mchambuzi wa masuala ya siasa, kijamii na kiuchumi, Philipo Mwakibinga, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufungua rasmi mkutano wa mahakimu na majaji kwa ujasiri na kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kulinda haki na misingi ya utawala wa sheria.
Akizungumza leo tarehe 14 Januari 2026 jijini Dar es Salaam, Mwakibinga alisema kauli za kizalendo zilizotolewa na Rais Samia zinaonesha dhamira ya kweli ya kuimarisha taasisi za haki nchini. Alieleza kuwa Rais alitoa maagizo mahsusi kwa serikali kuhakikisha inatekeleza wajibu wake kwa mahakama, huku akisisitiza umuhimu wa uhuru wa mahakama kuendana na uwajibikaji.
“Alitaka mahakama ilinde uhuru wake, na serikali ya Awamu ya Sita iendelee kuilinda mahakama. Hivyo anawasihi viongozi wa mahakama kuhakikisha uhuru huo unaambatana na uwajibikaji ili haki za wananchi zisimamiwe ipasavyo,” alisema Mwakibinga.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kulinda utu wa kila Mtanzania, akitoa wito kwa wananchi kuacha mijadala isiyo na tija na badala yake kujielekeza katika masuala ya maendeleo ya taifa.
Mwakibinga aliongeza kuwa kiongozi wa kweli hawezi kukiuka misingi ya haki na sheria, bali hufikiri kwa mapana kuhusu mustakabali wa taifa. Alisema maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila usimamizi madhubuti wa haki, na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha nia ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya mahakama.
Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan alieleza matarajio yake ya kuona mahakama za Tanzania zikigeuka kuwa mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine. Alisisitiza haja ya kuwa na msingi imara wa kisheria, na kueleza kuwa serikali imeanza kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
