TUZO ZA HALI YA HEWA 2026 KUWA CHACHU KWA WANAHABARI KUBORESHA UANDISHI WA HABARI ZA HALI YA HEWA
Dar es Salaam, Oktoba 22, 2026.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari, amesema Tuzo za Hali ya Hewa 2026 ni chachu kwa wanahabari kuongeza juhudi, ubunifu na ubora katika uandishi wa habari za hali ya hewa ili kusaidia kuelimisha umma na kuimarisha hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Jaji Bakari ameyasema hayo wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa wanahabari waliofanya vizuri katika uandishi wa habari za hali ya hewa kwa mwaka 2026, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), jijini Dar es Salaam, Oktoba 22, 2026.
Amesema tuzo hizo zinalenga kuhamasisha ushindani chanya miongoni mwa wanahabari na kuimarisha ushirikiano kati ya TMA na vyombo vya habari, ili kuhakikisha taarifa na tahadhari za hali ya hewa zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa lugha inayoeleweka.
Aidha, kabla ya hafla hiyo, TMA iliendesha warsha ya kuwajengea uwezo wa kitaalamu wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari. Warsha hiyo ilijadili mwelekeo wa mvua za msimu kuanzia Novemba 2026 hadi Aprili 2027 pamoja na hali ya El Niño.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Joseph Kulangwa, ameipongeza TMA kwa kutambua na kuthamini mchango wa wanahabari katika kuhabarisha umma kuhusu masuala ya hali ya hewa.
Kulangwa amesema tuzo hizo ni heshima na motisha kwa waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi kwa bidii, huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa TMA kwa kutambua mchango wa wanahabari katika jamii.
Vilevile, amewahimiza washindi na wanahabari ambao hawakupata tuzo kuendelea kujituma, kuboresha kazi zao na kuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha na kuhabarisha umma kuhusu taarifa za hali ya hewa.
Tuzo hizo zinatarajiwa kuendelea kuhamasisha uandishi wa habari unaozingatia ubora, weledi na umuhimu wa taarifa za hali ya hewa katika kusaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi na kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.








