TANZANIA YAONGOZA AJENDA ZA USAFIRI WA MAJINI KIKANDA
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Shirika la Usafiri wa Majini la Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOESNA) ni jukwaa muhimu la kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha usafiri wa majini na kuongeza mchango wake katika biashara na uchumi wa Afrika.
Akifungua mkutano huo jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha ushirikiano kwa kuunganisha miundombinu ya bandari, reli na barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo, kuongeza ajira na kukuza biashara katika ukanda huo.
Amesema Tanzania ina nafasi muhimu katika usafirishaji wa kikanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam, huku akieleza kuwa mkutano huo unatoa fursa kwa nchi wanachama kutathmini utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita uliofanyika Nairobi, Kenya, mwaka 2024 na kuweka mikakati mipya ya kukabiliana na changamoto za sekta hiyo.
Waziri Mkuu ametaja ajenda zinazojadiliwa kuwa ni pamoja na itifaki ya kikanda ya usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya majini, ushirikiano kati ya kampuni za usafirishaji pamoja na maandalizi ya kuanzisha Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri wa Majini kwa ajili ya elimu, utafiti na ubunifu.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Tanzania imepokea kwa dhamira ya dhati jukumu la kuongoza ushirikiano wa kikanda katika sekta hiyo, akieleza kuwa kipindi cha uenyekiti wa Tanzania kitalenga kuongeza ushiriki wa nchi za Afrika katika umiliki na uendeshaji wa meli, kuendeleza wataalamu na kukuza uchumi wa buluu.
Naye Katibu Mkuu wa MOESNA, Kassim Mpaata, amesema takribani asilimia 88 ya biashara ya kimataifa husafirishwa kwa njia ya bahari, lakini sehemu kubwa ya shughuli hizo inadhibitiwa na kampuni za meli zinazomilikiwa na wageni, hali inayofanya nchi za Afrika kukabiliwa na gharama kubwa za usafirishaji na kupoteza sehemu ya mapato ya sekta hiyo.
Amesema MOESNA inaendelea kuhimiza nchi wanachama kuunganisha rasilimali na utaalamu ili kuongeza ushiriki wa Waafrika katika umiliki na uendeshaji wa meli, ujenzi na ukarabati wa meli, pamoja na kuimarisha usalama wa majini, ulinzi wa mazingira na mafunzo ya wataalamu wa sekta hiyo.






