STAMICO YANG'ARA MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA, YANYAKUA TUZO TANO
Na Mwandishi wetu,GEITA:
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeibuka na ushindi wa tuzo tano katika siku ya kwanza ya utoaji wa tuzo za Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika eneo la Bombambili, mkoani Geita.
Mafanikio hayo yanaonesha kutambuliwa kwa mchango wa STAMICO katika kukuza sekta ya madini nchini, hususan katika kuwawezesha wachimbaji wadogo, kuhamasisha ubunifu na kuendeleza matumizi ya nishati safi.
Tuzo hizo zimetolewa Septemba 2, 2026, na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Latifa Khamis, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Khamis aliipongeza STAMICO kwa juhudi zake za kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuunga mkono utunzaji wa mazingira kupitia ubunifu wa nishati safi, hususan utengenezaji wa mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes unaolenga kupunguza matumizi ya kuni na ukataji wa miti.
Aidha, Kijiji cha STAMICO kimeendelea kuvutia wadau mbalimbali wa sekta ya madini kutokana na ubunifu wake na namna kilivyowashirikisha makundi mbalimbali, yakiwemo wachimbaji vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano ya Umma wa STAMICO, Deus Alex Ntukamazina, alisema tuzo hizo ni chachu kwa shirika kuendelea kuongeza juhudi katika kutekeleza majukumu yake na kushirikiana na wadau wa sekta ya madini.
Ntukamazina alieleza kuwa STAMICO itaendelea kuwekeza katika mnyororo mzima wa thamani wa madini, kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa lengo la kuongeza tija na kuchangia maendeleo ya taifa.
Aliongeza kuwa shirika hilo limejipanga kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali ili kukuza shughuli za uchimbaji, kuongeza uzalishaji na kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, STAMICO inaendelea kuonesha jitihada za kuunganisha teknolojia, ubunifu, ushirikishwaji wa makundi mbalimbali na utunzaji wa mazingira katika kukuza sekta ya madini nchini.


