Breaking News

SERIKALI YAONGEZA NGUVU UWEKEZAJI WA NISHATI SAFI

 

Na Hawa Ismail – Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, Juma Homera, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau mbalimbali katika kuimarisha uwekezaji wa nishati safi na kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Akizungumza katika Maonesho na Mkutano wa 10 wa Nishati (Power and Energy Trade Expo) uliofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Homera amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa umeme ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

Amesema kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) kumeongeza megawati 2,115 kwenye Gridi ya Taifa, huku Mradi wa Nishati ya Jua wa Kishapu ukiingiza zaidi ya megawati 50 na mikataba mipya ikiendelea kuwezesha uzalishaji wa takriban megawati 100 zaidi.

Kwa mujibu wa Homera, Wizara ya Nishati imetenga zaidi ya Sh trilioni 2.4, sawa na asilimia 97.5 ya bajeti ya wizara hiyo, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya umeme na nishati.

Amesema baada ya kufanikisha kwa kiasi kikubwa usambazaji wa umeme vijijini, Serikali imeendelea na mpango wa kupeleka umeme katika vitongoji zaidi ya 9,009 nchini, huku ikilenga kuongeza uzalishaji wa umeme hadi kufikia megawati 8,000 na kuunganisha wateja zaidi ya milioni 8.3 ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Chama cha Nishati Tanzania (TEA), Emmanuel Michael, amesema sekta hiyo inahitaji ushirikiano mpana kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuongeza uwekezaji, kuhamisha teknolojia na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani, akisisitiza matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati kama jua, upepo na biogesi.

Aidha, Serikali imewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya nishati, ikiwemo ujenzi wa vituo vya kuchajia magari ya umeme, miradi ya gesi asilia na nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya kufikia lengo la kuwawezesha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi.